Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Kahama, Elias Kuandikwa (kulia) na msaidizi wake Ezekiel Maige (katikati) muda mfupi baada ya kusimikwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mwigulu Nchemba kuwa makamanda wa UVCCM Kahama.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mwigulu Nchemba akiwahutubia wana CCM mjini Shinyanga muda mfupi baada ya kusimika makamanda wa UVCCM mkoani Shinyanga.
IMEELEZWA kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kuendelea kuongoza nchi kwa kipindi kirefu zaidi iwapo vijana wake (UVCCM) watasimama kidete katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, kanuni na mipaka ya kazi zao.
 
Hayo yamebainishwa na mmoja wa makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Elias Kuandikwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga muda mfupi baada ya kusimikwa kuwa kamanda wa vijana wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
 
Kuandikwa alisema chama chochote cha siasa duniani hutegemea zaidi nguvu za vijana wake ambao wanapaswa kuhakikisha wanakinadi  kwa wananchi kwa kuzieleza kwa ufasaha sera na ilani yake ya uchaguzi ili kiendelee kukubalika na kuongoza dola kwa kipindi kirefu.
 
Alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani vijana ndiyo wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwanadi wagombea wa CCM kwa wananchi na kuelezea mambo yote mazuri ya maendeleo yaliyokwishafanyika maeneo mengi nchini chini ya serikali ya CCM.
 
“Nitumie fursa hii kuwaomba vijana wote wa CCM hapa mkoani kwetu wahakikishe wanasimama kidete kukipigania chama chao pamoja na kuteleza shughuli zote za chama kikamilifu, waelewe wao ndiyo nguzo muhimu ndani ya chama, ni wapiganaji wa kwanza katika mambo yote hivyo wasibweteke, kujihesabu tu kuwa ni vijana wa CCM, haitoshi,”
 
“Lazima waoneshe vitendo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, sisi vijana ndiyo tuwe mstari wa mbele katika kunadi sera za chama chetu na ilani yetu ya uchaguzi, nina imani tukitimiza wajibu wetu, CCM itaendelea kuongoza hata milele,” alieleza Kuandikwa.
 
Kwa upande mwingine kamanda huyo wa vijana aliwaomba viongozi wengine ndani ya chama kuacha tabia ya kuwatumia vijana kwa muda wakati wa vipindi vya uchaguzi ambapo uzoefu unaonesha mara baada ya uchaguzi hizo kukamilika huwaacha solemba bila ya kuwawekea mazingira yatakayowawezesha kufanya kazi.
 
“Pamoja na kuwataka vijana wawe mstari wa mbele katika kukitetea chama lakini pia ni vyema kwa viongozi wetu wakuu ndani ya chama wawe na mipango madhubuti ya kuwasaidia vijana hawa ambayo itawawezesha wawe na shughuli za kuwaingizia kipato hasa pale wanapomaliza majukumu muhimu wakati wa uchaguzi,” alieleza.
 
Akizungumza kuhusu viongozi watakaochaguliwa kwa tiketi ya CCM kuongoza serikali ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kutekeleza ahadi zote  wanazitoa hivi sasa kwa wananchi kupitia mikutano ya kampeni na kwamba kiongozi bora ni yule anayetimiza wajibu wake kwa waliomchagua.
 
Kuandika alisema kiongozi anaposhindwa kutekeleza wajibu wake ndiyo chanzo cha wananchi kukichukia chama kinachoongoza serikali na kwamba yeye binafsi atatumia nafasi aliyopewa ya ukamanda wa vijana kuhakikisha viongozi wote katika wilaya yake wanatimiza wajibu wao kama walivyoahidi kwa wananchi.
 
Mwisho.
 
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top