Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga Khamis Mgeja katika moja ya mikutano yake na wana CCM. |
Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akizungumza na wana CCM wa matawi ya Nhelegani na Busalala kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga. |
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma na mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Shinyanga, Charles Gishuli akizungumza na wana CCM wa matawi ya Nhelegani na Busalala. |
Wana CCM wa Matawi ya Busalala na Nhelegani wakimsikiliza mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja. |
IDADI kubwa ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za mitaa kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi ujao nchini imetajwa kuwa ni dalili njema za ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo.
Hali hiyo imebainishwa na mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alipokuwa akizungumza na wanachama wa matawi mawili ya CCM ya Nhelegani na Busalala kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga ambapo alisema wingi wa wagombea waliojitokeza unaonesha wazi bado watanzania wana imani kubwa na CCM.
Mgeja alisema kujitokeza kwa wagombea wengi katika zoezi la upigaji wa kura za maoni kunaashiria wazi bado chama hicho kinakubalika vizuri hapa nchini na ni dalili za kupata ushindi wa kishindo kwa wagombea wake wote katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika nchini kote Desemba 14, mwaka huu.
“Binafsi nimeridhishwa na jinsi wana CCM mlivyojitokeza kuomba kugombea nafasi mbalimbali za serikali za mitaa kwa tiketi ya CCM, imeonesha bado mna imani na chama chenu, ni chama ambacho watanzania wanakiheshimu, endeleeni kukiunga mkono, wingi wenu ni dalili za ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,”
“Imani hii inadhihirisha jinsi CCM inavyowatekelezea wananchi wake miradi mbalimbali ya maendeleo, na daima itasimamia utekelezaji wa ahadi zake inazozitoa mara kwa mara kwa watanzania japokuwa wapo wanaoendelea kutubeza wakidai hakuna kinachofanyika, hawa ni wa kupuuzwa, na nina wasiwasi huenda akili zao zina upungufu fulani,” alieleza Mgeja.
Kwa upande wake mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Shinyanga, Charles Gishuli aliwataka wana CCM wote kurejesha mshikamano waliokuwa nao hapo awali kabla ya zoezi la upigaji wa kura za maoni kwa kuhakikisha wanawanadi wanachama wenzao walioteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa mapema mwezi ujao.
Gishuli ambaye hivi sasa ni mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma aliwaomba wana CCM waache tabia ya kuchafuana wenyewe kwa wenyewe kwa vile kitendo hicho kina madhara makubwa kwa chama chao wakati wa kampeni za chaguzi zitakazohusisha pia wagombea kutoka vyama vya upinzani.
Gishuli alisema wana CCM walioomba kugombea nafasi mbalimbali katika serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kwa tiketi ya CCM wametumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi na kwamba ndani ya CCM hakuna mgombea anayeshindwa bali chaguzi za ndani huwa ni kwa ajili ya kupangana tu.
“Ni muhimu baada ya upigaji kura za maoni wana CCM wote tushikamane na kuwa kitu kimoja, tuvunje kambi tulizokuwa nazo kwa kuziunganisha pamoja ili tuwanadi wagombea wetu kwa nguvu moja waweze kuibuka na ushindi katika chaguzi zijazo, tuache kuchafuana wenyewe kwa wenyewe, maana tunaweza kuwapa faida wapinzani,” alieleza Gishuli.
Post a Comment