JESHI
la Zimamoto na Uokoaji nchini limewaomba wananchi kuacha kutoa lawama dhidi
yake kila pale panapotokea janga la moto na badala yake walisaidie kwa
kuishinikiza serikali itatue changamoto kadhaa zinazolikabili ili liweze
kufanya kazi zake kwa ufanisi mzuri.
Ombi
hilo limetolewa na Kamishna Mkuu wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji nchini, Pius Nyambacha alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari mjini Shinyanga muda mfupi baada ya kuwasili mkoani humo kukagua
shughuli za jeshi hilo.
Nyambacha
alisema kwa kipindi kirefu Jeshi la Zimamoto limekuwa likilaumiwa kwa uzembe
kutokana na kushindwa kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo mengi nchini
ambapo hata hivyo jamii haichunguzi kwa kina chanzo chake na badala yake hubaki
wakilalamika kulaumu.
Alisema
zipo changamoto nyingi zinazolikabili Jeshi lake na hivyo kushindwa kufanya
kazi zake kwa ufanisi ikiwemo suala la uhaba wa maeneo ya kuongezea maji mijini
pale linapotokea tatizo la nyumba kuungua moto kutokana na kuhitajika kwa maji
mengi ili kuweza kukabiliana na moto.
“Yapo
mambo mengi ambayo tunaamini wenzetu wananchi hawayaelewi na hivyo kila mara
kutushushia lawama kwamba sisi ni wazembe, ukweli tunajitahidi sana, sasa
tuwaombe wenzetu wana habari mtusaidie kuielimisha jamii ili iweze kuwa na
uelewa wa kutosha jinsi tunavyofanya hii kazi hasa upande wa uzimaji wa moto,”
“Zipo
changamoto nyingi zinazotukabili hasa tatizo la uhaba wa maeneo ya kuongezea
maji katika sehemu nyingi za miji yetu, wananchi wanapaswa waelewe kuwa magari
yetu hutumia lita 2000 za maji ndani ya dakika mbili yanapozima moto, hivyo
yanapomalizika lazima tuongeze mengine,” alieleza Nyambacha.
Akifafanua
magari mengi yaliyopo nchini hayana uwezo wa kuchukua maji mengi zaidi hivyo
yanapomalizika hulazimika kurudi katika eneo la kujazia maji na mara nyingi
maeneo hayo yanakuwa mbali na eneo la tukio la moto na kwamba ndiyo sababu ya
wananchi kulalamika kwamba zimamoto walikwenda bila maji.
“Hili
ni tatizo kubwa sana, sisi wenyewe hatupendi iwe hivyo, laiti miji yetu
ingekuwa na utaratibu wa kujenga (viosk) vingi mitaani kwa ajili ya magari yetu
kujazia maji tungeweza kukabiliana vizuri na majanga ya moto yanayotokea katika
maeneo yetu, lakini pia lipo tatizo la uchakavu wa magari, hili linafanyiwa
kazi na serikali,” alieleza.
Kwa
upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani Shinyanga, Elias Mugisha
aliiomba serikali iuongezee mkoa wake askari wa kutosha ili kuweza kufanya kazi
zao kwa ufanisi ambapo alisema mpaka sasa mkoa huo una askari 41 katika wilaya
zote ikiwemo na viwanja vya ndege vya Ibadakuli na Kahama.
Post a Comment