Naibu Katibu Mkuu wa CCM - Zanzibar, Vuai Ali Vuai akionesha sehemu ya kadi za CHADEMA zilizorejeshwa na wagombea wa chama hicho ambao wameamu kurejea CCM.
Inavyoelekea Naibu Katibu Mkuu, Vuai Ali Vuai anashangazwa na nguvu ya Chama chake jinsi kinavyosambaratisha wapinzani.
Tupo Imara - Hakuna wa kuchezea Chama chetu.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga vijijini na Kishapu kufanikiwa kuisambaratisha kambi ya Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA) baada ya wagombea wake wengi kujitoa kuwania nafasi mbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.


Hatua hiyo imewawezesha wagombea wengi wa CCM kupita bila kupingwa baada ya kukosa wapinzani hasa katika nafasi za wenyeviti wa vijiji na vitongoji wakiwemo pia wajumbe wa serikali za vijiji na vitongoji ambapo mpaka juzi CCM Shinyanga vijijini ilikuwa imepita bila kupingwa katika zaidi ya vitongoji 200.

Baadhi ya waliokuwa wagombea kwa tiketi ya CHADEMA katika jimbo la Solwa walijitokeza katika mkutano wa kampeni za CCM ambao mgeni wake rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Vuai Ali Vuai na kutangaza rasmi kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na kurejea CCM.

Mmoja wa wagombea wa CHADEMA aliyejitokeza katika mkutano wa hadhara Kata ya Iselamagazi, Sosoma Francis alisema ameamua kujitoa kugombea nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kadata baada ya kukaa na kutafakari kwamba hatua yake ya kugombea nafasi hiyo ilitokana na kushawishiwa na viongozi wa CHADEMA.

“Mheshimiwa Naibu Katibu mkuu nimekuja hapa mbele yako kukukabidhi kadi ya CHADEMA baada ya kujitoa kugombea katika nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kadata, maana viongozi wa CHADEMA walikuwa wamenilazimisha nigombee, lakini nimeona kuna ubabaishaji mkubwa hivyo nimejitoa na kurejea CCM,”  alieleza Francis.

Pia katika mkutano huo wanachama 31 wa CHADEMA  waliamua kurejesha kadi zao na kujiunga na CCM ambapo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar aliwapongeza kwa uamuzi wao huo na kuwaomba wana CCM wengine kuwapokea na kuwapa ushirikiano wa kutosha hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa nchini.

“Nakupongezeni sana kwa uamuzi wenu wa kurejea CCM, hiki ni chama makini chenye sera zinazotekelezeka ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa hapa nchini, hakina tabia ya fujo wala matusi, badala yake kimejikita zaidi katika kuwaletea maendeleo wananchi kinaowaongoza,”

“Kazi kubwa ya CCM ni kuhakikisha nchi yetu daima inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu muda wote maana bila ya amani hakuna kazi yoyote ya maendeleo au ya kijamii itakayoweza kufanyika, tuwaepuke wenzetu wote wanaoanzisha chokochoko zinazoweza kusababisha kutoweka kwa hali hiyo nchini kwetu,” alieleza Vuai.
 
Naibu Katibu mkuu wa CCM - Zanzibar, Vuai Ali Vuai akiwasili katika eneo la mkutano wa hadhara wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Wilayani Kishapu zaidi ya wanachama  10 wa CHADEMA wakiwemo waliokuwa wakigombea nafasi za ujumbe wa serikali za vitongoji katika serikali ya kijiji cha Mwashinonghela na Kitongoji cha Mwamanonga  walirejesha kadi za chama chao na kujiunga na CCM katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika juzi kijiji cha Mwashinonghela.

Wanachama hao walikabidhi kadi zao kwa diwani wa Kata ya Seke Bugoro, Ferdinand Mpogomi ambapo walisema wameamua kwa hiari yao kujiunga na CCM baada ya kutoridhishwa na nyendo za viongozi wa CHADEMA ambao muda wote hawatoi ushirikiano kwa wanachama wao wa ngazi za chini.


Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top