Bariadi

HATIMAYE Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bariadi mkoani Shinyanga kimefanikiwa kwa mara ya kwanza kuunda Halmashauri ya wilaya ya Bariadi baada ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini.

Chama cha United Democratic (UDP) ndicho kilichokuwa kikiunda uongozi wa Halmashauri hiyo ya wilaya tangu mwaka 1995 ambapo kiliibuka kidedea katika uchaguzi huo wa kwanza kwa kukibwaga Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuendelea kutamba katika chaguzi mbili zilizofuata za mwaka 2000 na 2005.

Mafanikio hayo ya CCM yamekuja baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu nchini ambapo chama hicho kilifanikiwa kupata madiwani 26 huku Chama cha UDP kikiambulia madiwani 21 na hivyo kutoa nafasi kwa CCM kuweza kuongoza Halmashauri hiyo ya wilaya kwa mara ya kwanza.

Katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya uliofanyika juzi mjini Bariadi Bw. Mabula Bahati Magamula (CCM) alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo ambapo Bw. Daud Nyalabu kutoka kata ya Mbita alichaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti.

Huko wilayani Kishapu aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Bw. Boniface Butondo alijikuta akishindwa kurejea katika wadhifa wake huo baada ya kushindwa katika kura za maoni za madiwani wa CCM alipoangushwa kura hizo na mpinzani wake wa muda mrefu Bw. Justin Sheka.

Katika uchaguzi rasmi wa baraza la madiwani uliofanyika juzi wilayani Kishapu Bw. Sheka aliibuka na ushindi baada ya kumshinda mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Masunga Pengwa.

Kwa upande wake Bw. Samson Gelewa alichaguliwa kuwa Naibu mwenyekiti katika Halmashauri hiyo ya wilaya ya Kishapu wakati huko wilayani Shinyanga Bw. Amos Mshandete pamoja na Naibu wake Bw. George Lunyembeleka walifanikiwa kutetea nafasi zao kwa kupita bila kupingwa huku pia wakiungwa mkono na diwani kutoka Chama cha Wananchi (CUF).


Bw. Gulam Mukadam alichaguliwa kuwa Meya mpya wa baraza la madiwani katika Manispaa ya Shinyanga baada ya kupita katika mnyukano mkali uliokuwepo awali katika kura za maoni za kamati ya madiwani wa CCM wa manispaa hiyo huku Bi. Agnes Machiya akichaguliwa kuwa naibu meya pia mpya.

Wilayani Meatu Bw. Pius Machungwa pia aliweza kurejeshwa katika nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa miaka mingine mitano ambapo Bw. Bassu Kayungilo alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti.

Naye Bw. Steven Dwese aliibuka na ushindi huko wilayani Maswa baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa halmashauri ya wilaya hiyo ambapo naibu meya aliyechaguliwa ni Bw. Ndila Mayeka kutoka kata ya Kadoto.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top