HALMASHAURI YA WILAYA YA NZEGA YAPIGA HATUA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.
MOJA ya vipaumbele vilivyoainishwa ndani ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 ni suala la uboreshaji wa sekta ya afya nchini hasa maeneo ya vijijini.
Suala la afya limepewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake hasa ikizingatiwa kuwa Taifa lolote linalotaka kupiga hatua katika suala zima la maendeleo ni lazima wananchi wake wawe na afya bora.
Kifungu cha 86 ndani ya ilani hiyo ya uchaguzi kinaelezea mipango na mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na serikali inayoongozwa na CCM katika suala zima la uboreshaji wa sekta ya afya.
Katika kifungu hicho kuwa imeelezwa kuwa, nanukuu, “…..Maendeleo ya Taifa letu yataletwa na wananchi wenye afya bora inayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali. Katika miaka mitano ijayo, serikali itatekeleza na chama kitatoa kipaumbele katika maeneo yaliyoainishwa katika MKUKUTA na Malengo ya millennia.”
Moja ya mambo yaliyopangwa kutekelezwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango wa maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ambao unazingatia na kutoa kipaumbele katika maeneo ya upatikanaji wa raslimaliwatu wenye ujuzi na wa kutosha katika sekta ya afya.
Pia kuhakikisha uwepo wa miundombinu ya huduma za afya na ustawi wa jamii kwa kukarabati na kujenga vituo vya kutolea huduma katika afya, ustawi wa jamii hasa ngazi ya kijiji na kata na kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, tiba na vitenganishi katika vituo vya kutolea huduma na uimarishaji mfumo wa rufaa kutoka vijijini hadi taifa.
Kutokana na hali hiyo CCM katika kuhakikisha ahadi zake ilizozitoa kwa wananchi zinatekelezwa baada ya kuunda serikali iliwakabidhi rasmi ilani hiyo ya uchaguzi watendaji wake katika ngazi ya serikali kuu na serikali za mitaa ili iweze kutekelezwa kwa vitendo.
Mbali ya kuwakabidhi watendaji wa serikali ilani hiyo lakini pia wawakilishi wa wananchi wanaotokana na CCM wakiwemo wenyeviti wa serikali za vijiji, madiwani na wabunge walielekezwa kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezwaji wa ilani hiyo ili kukiwezesha chama hicho kiendelee kukubalika nchini.
Halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora ni moja ya halmashauri nchini zilizopiga hatua ya kuridhisha katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ambapo mpaka hivi sasa imeweza kutekeleza mipango mingi ya maendeleo kwa wananchi wake.
Moja ya eneo lililoonesha mafanikio ni la sekta ya afya kwa jamii ambapo ujenzi wa zahanati zenye majengo ya kisasa katika vijiji kadhaa umefanyika hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kusogeza karibu huduma za afya kwa jamii husika.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa za mwaka 2012 wilaya ya Nzega ina jumla ya wakazi 502,252 kati yao wanaume ni 245,003 na wanawake wakiwa ni 257,249 ambapo kiutawala ina jumla ya tarafa nne za Nyasa yenye kata 12, vijiji 56 na vitongoji 329.
Tarafa nyingine ni Puge yenye kata tisa, vijiji 39 na vitongoji 335. Bukene yenye kata nane ikiwa na jumla ya vijiji 36 na vitongoji 191 na tarafa ya nne ni ya Mwamalundi ambayo ina kata nane zenye vijiji 36 na vitongoji vyake vikiwa ni 152.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita halmashauri hiyo imeweza kujenga zahanati kadhaa ambapo hivi sasa ina jumla ya zahanati 36 zinazomilikiwa na halmashauri yenyewe ambapo pia zipo zahanati tatu za watu binafsi na tatu nyingine zikiongezwa na mashirika ya kidini.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nzega, Abdulrahaman Mndeme anasema katika kuhakikisha suala la uboreshaji wa huduma za afya katika halmashauri yake linapewa kipaumbele walifanya kila juhudi ya kuihamasisha jamii kuona umuhimu wa kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa zahanati katika maeneo yao.
Mndeme anasema kutokana na hamasa iliyofanyika hivi sasa sehemu kubwa ya zahanati zilizojengwa zimeanza kufanya kazi na kwamba ni zahanati moja tu ambayo haijaanza kufanya kazi ambapo hata hivyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za usajili wake ili ianze kazi.
“Kwa kweli katika suala la uboreshaji wa huduma za afya hatua tuliyopiga ni ya kuridhisha, tumejitahidi kusogeza karibu huduma kwa wananchi wetu, halmashauri yetu mpaka sasa tunazo zahanati 36 zinazoendeshwa na serikali, lakini pia wenzetu wa madhehebu ya kidini wanamiliki zahanati tatu,”
“Pia watu binafsi wanazo zahanati tatu, kwa hizi zilizojengwa na halmashauri tayari zinafanya kazi vizuri, ni moja tu iliyoko kijiji cha Shigamba ambayo ujenzi wake ulikamilika hivi karibuni ndiyo haijaanza kazi, lakini tunatarajia itaanza kazi wakati wowote baada ya taratibu za kuisajili kukamilika,” anasema Mndeme.
Mndeme anasema mbali ya uwepo wa zahanati hizo pia halmashauri yake ina vituo sita vya afya ambavyo vinne vinaendeshwa na halamshauri yenyewe kituo kimoja kinamilikiwa na Shirika la dini na kingine ni cha mtu binafsi ambavyo vyote vina lengo moja la kuwahudumia wakazi wa wilaya ya Nzega.
“Tunayo hospitali moja ya wilaya inayomilikiwa na serikali na nyingine inamilikiwa na Shirika la dini iliyopo Nkinga, hospitali hizi pamoja na vituo vingine vya kutolea huduma za afya zimewezesha wananchi wetu kutokuwa na matatizo makubwa katika kupata huduma za matibabu.
Hata hivyo mkurugenzi huyo anasema kila penye mafanikio hapakosi kuwepo changamoto mbalimbali ambapo kwa upande wa sekta ya afya changamoto kubwa ni tatizo la uhaba wa watumishi hasa madaktari bingwa, madaktari wanaopaswa kutoa huduma katika zahati zilizojengwa pamoja na wauguzi.
Changamoto nyingine iliyotajwa ni uhaba wa dawa katika zahanati zilizopo vijijini na wakati mwingine katika hospitali yetu ya wilaya ambapo hata hivyo alisema tatizo kubwa ni upatikanaji wake kutoka bohari kuu la serikali linashughulikia usambazaji wa dawa nchini (MSD).
SEKTA YA ELIMU.
Kwa upande wa sekta ya elimu Mndeme anasema halmashauri yake katika eneo la shule za sekondari hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2012 ilikuwa na sekondari 39 zinazomilikiwa na serikali ambapo mashirika ya dini yanamiliki sekondari tatu.
“Katika kuboresha shule zetu za sekondari, mpaka hivi sasa tumefanikiwa kujenga maabara 20 katika shule 12, ambapo 16 zipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji, lakini pia kwa upande wa hosteli tayari shule tatu zimeishajengewa hosteli, shule hizo ni sekondari ya Puge, Nata na ile ya Hamza Aziz Ally,”
“Lakini pia kama ilivyoelezwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo sisi watendaji tulikabidhiwa kuitekeleza wilaya yetu imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa elimu ya msingi mpaka sasa tuna shule za msingi 171 kati ya hizo 169 ni za serikali na mbili zinamilikiwa na watu binafsi,” anasema Mndeme.
Hata hivyo anasema kutokana na ongezeko la idadi ya watu katika halmashauri hiyo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa msongamano mkubwa wa watoto madarasani katika shule mbalimbali za msingi hali ambayo imesababisha halmashauri ilazimike kujenga shule mpya katika eneo la Ipilili mjini Nzega.
“Msongamano wa wanafunzi katika shule zetu za msingi hasa eneo la hapa mjini Nzega ilisababisha tuchukue uamuzi wa kujenga shule mpya ya msingi katika eneo la Ipilili, shule hii imejengwa kwa msaada wa fedha kutoka mfuko wa maendeleo (LGCGD), imetugharimu kiasi cha shilingi milioni 29.1,” anasema Mndeme.
Anasema pia hivi sasa halmashauri yake inafanya kila juhudi kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama shuleni linapatiwa ufumbuzi ambapo tayari sekondari moja ya Undoma imechimbiwa kisima kimoja kirefu na kupunguza tatizo hilo.
“Kisima hiki kilichochimbwa katika sekondari ya Undoma mbali ya kuwasaidia watoto wanaosoma katika kijiji hicho lakini kwa kiasi kikubwa kimepunguza tatizo la maji katika vijiji jirani vinavyoizunguka shule hiyo, baadhi ya shule kwa hivi sasa tumezijengea matanki yanayotumika kuvuna maji ya mvua, yamesaidia sana,” anasema Mndeme.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI.
Kwa upande wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kama inavyoelezwa ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM kwamba moja ya mambo yatakayopewa kipaumbele katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja kuwawezesha wananchi wenyewe kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi yao.
Ilani hiyo ya uchaguzi ilibainisha kuwa moja ya tatizo la wananchi kushindwa kupiga hatua katika suala zima la kiuchumi ni ukosefu wa mitaji hivyo ilani hiyo inaelekeza hatua mbalimbali za kuwasaidia wananchi ili kuweza kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao.
Wilaya ya Nzega katika kutekeleza eneo hilo la kiuchumi katika kipindi cha mwaka 2007/2008 hadi 2012/2013 iliweza kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya wanawake inayofikia kiasi cha shilingi 202,000,000 ambapo kwa pia katika kipindi hicho vikundi vya vijana vilipatiwa mikopo ya shilingi 54,300,000.
“Tumejitahidi sana katika kuviwezesha vikundi vya wanawake na vijana kwa kuwapatia mikopo ili viweze kuinua mitaji yao, hali ya marejesho siyo mbaya sana japokuwa upande wa wanawake ndiyo unaosuasua katika urejeshaji,”
“Hata hivyo katika kuhakikisha vikundi hivi vinaendelea kuwa imara tumekuwa tukiwashauri wanachama wake kujianzishia vyama vyao vya akiba na mikopo (SACCOS), wilaya yetu mpaka sasa ina vyama vya ushirika 115 kati yake 51 ni vya mazao, SACCOS ni 44 na 20 vikiwa ni vya mchanganyiko,” anasema Mndeme.
Mwisho.
Post a Comment