MWAKILISHI WA MKURUGENZI MTENDAJI TASAF MAKAO MAKUU, ALPHONCE KYARIGA AKITOA MADA KATIKA WARSHA YA KUJENGA UELEWA KWA VIONGOZI, WATENDAJI NA WAWEZESHAJI WILAYANI MBOGWE, MKOA WA GEITA.
MPANGO wa kunusuru kaya maskini nchini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu umelenga kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri miongoni mwa watanzania wapatao milioni 14 angalao kwa asilimia 50 ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo.

Hali hiyo imebainishwa na mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa TASAF Taifa, Alphonce Kyariga katika ufunguzi wa warsha ya siku moja ya kujenga uelewa kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini nchini kwa viongozi, watendaji na wawezeshaji wilayani Mbogwe mkoani Geita.

Kyariga alisema kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu umelenga kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri miongoni mwa watanzania kwa kuzipatia kaya zenye hali duni fedha taslimu ili ziweze kujipatia mahitaji muhimu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Akifafanua alisema mpango huo uliopangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa awamu mbili za miaka mitano mitano haulengi kuwafanya walengwa kuwa tegemezi bali utahakikisha katika kipindi cha utekelezwaji wake pia wahusika wanajengewa uwezo ili waweze kujitegemea ambapo misaada hiyo itatolewa kwa kaya husika kwa miaka mitatu pekee.

“Takwimu zilizopo hapa nchini zinaonesha  takriban watanzania milioni 14 wanaishi katika umaskini uliokithiri, hivyo basi mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia TASAF awamu ya tatu umelenga kupunguza idadi hiyo angalao ifikie nusu yake baada ya miaka 10 ijayo,”

“Mpango umelenga kuziwezesha kaya hizi ziweze kuishi katika hali nzuri, lakini pia utashughulikia hali iliyosababisha ziwe na hali hiyo ngumu ambapo katika miaka mitano ya kwanza ya mpango huu baadhi ya shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kuzitambua, kuzisajili na kuziainisha kaya hizo maskini,” alieleza Kyariga.

Alisema TASAF awamu ya tatu itatoa ruzuku za aina mbili kwa kaya zenye hali duni na zenye kuishi katika mazingira hatarishi ambazo ni ruzuku ya msingi na ile itakayotegemea kutimiza masharti ya elimu na afya ambapo  patakuwepo pia na miradi itakayotoa ajira za muda kwa walengwa.

“Miradi ya ajira za muda ni sehemu mojawapo ndani ya mpango wa kunusuru kaya maskini, madhumuni ya miradi hii ni kutoa fursa za ajira ya muda kwa walengwa ili kuongeza kipato na matumizi kwenye kaya, kujenga na kuimarisha miundombinu katika jamii, na kuongeza ujuzi kwa walengwa,” alieleza Kyariga.

Kwa upande wake mkuu mpya wa mkoa wa Geita, Fatuma Mwasa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na katibu tawala wa wilaya ya Mbogwe, Julius Gerald aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuhakikisha wanazingatia mafunzo yatakayolewa kwa lengo ili kufanikisha mpango huo katika maeneo yao.

“Ndugu viongozi mnaoshiriki katika warsha hii, mafunzo haya ni muhimu sana kwenu, lakini pia mnapaswa muelewe kuwa hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 hivyo ni vizuri muhahikishe mpango huu unafanikiwa kwa lengo la kuwasaidia walengwa,”

“Ninyi viongozi mkiwemo waheshimiwa madiwani hakikisheni mnakuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yenu na wilaya nzima ya Mbogwe, tendeni haki katika utekelezaji wa mpango huu, simamieni kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili lengo liweze kufikiwa,” ilieleza sehemu ya hotuba ya mkuu wa mkoa.

Akiwasilisha mada kuhusu mpango wa kujenga uwezo wa kujikimu, mmoja wa wawezeshaji kutoka TASAF makao makuu, Barnabas Mkumbo alisema mpango huo utafanya kazi katika maeneo ambayo yana upungufu wa huduma za afya, elimu na maji kwa kuzingatia sera na viwango vya sekta husika.

“Mpango huu umelenga kuhamasisha walengwa kuweka akiba, kutekeleza shughuli za kiuchumi na kujiunga katika vikundi, kuvipatia zana muhimu kwa ajili ya kuweka akiba, kutoa mafunzo na kuviunganisha vikundi na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuweza kukuza uwezo wao kifedha,” alieleza Mkumbo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top