Ofisa uwezeshaji kutoka TASAF Makao Makuu, Barnabas Mkumbo akiwajibika.
Sehemu ya washiriki (wawezeshaji) walioshiriki katika warsha hiyo ya siku moja iliyofanyika Kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe mkoa wa Geita.
Mmoja wa madiwani wiayani Mbogwe akiuliza swali.
Maofisa kutoka TASAF Makao Makuu wakitoa mafunzo ya uelewa kwa viongozi, watendaji na wawezeshaji kuhusu Mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani Mbogwe.
MADIWANI katika halmashauri ya wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, wameagizwa kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini katika kata zao unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu ili kuhakikisha walengwa wote wananufaika na mpango huo.

Agizo hilo limetolewa wilayani Mbogwe na mkuu wa mkoa wa Geita, Fatuma Mwasa katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha ya siku moja ya kujenga uelewa kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini kwa viongozi, watendaji na wawezeshaji watakaosimamia mpango huo.

Mwasa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na katibu tawala wa wilaya ya Mbogwe, Julius Gerald, alisema viongozi wote watakaohusika katika utekelezaji wa mpango huo wanapaswa kutenda haki katika kuzibaini kaya maskini na kuondoa upendeleo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

“Ndugu zangu viongozi, hasa waheshimiwa madiwani wetu, hakikisheni mnatenda haki katika utekelezaji wa mpango huu, msitangulize upendeleo kwa kuzipendelea kaya zisizostahili na ambazo hazina walengwa au kutanguliza mbele maslahi binafsi, mkifanya hivi ni wazi lengo la mpango huu halitafikiwa,” ilieleza sehemu ya hotuba ya mkuu huyo wa mkoa.

Naye mmoja wa wawezeshaji kutoka TASAF makao makuu, Barnabas Mkumbo alisema utekelezwaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini na zenye maisha duni umelenga kuziwezesha kaya hizo ziweze kujipatia matumizi muhimu kwa njia endelevu, kuwa na matumizi wakati wa hari na kuimarisha shughuli za kujiongezea kipato.

Mkumbo alisema mpango huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano umelenga kuzifikia kaya zipatazo milioni moja zinazoishi katika hali ya  umaskini uliokithiri kwa kuziwezesha kujiongezea kipato kupitia uwekaji akiba na shughuli za kiuchumi ili kuziboreshea maisha.

“Mpango wa kunusuru kaya maskini utatoa ruzuku kwa kaya maskini sana hususani zenye wajawazito na watoto ili ziweze kupata huduma za elimu na afya, kutoa ajira kwa kaya zitakazokuwa na watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa majanga mbalimbali kwa mfano, ukame na mafuriko,” alieleza Mkumbo.

Akifafanua kuhusu ajira kwa kaya maskini, alisema zitatolewa kwa kaya zitakazokuwa na watu wenye uwezo wa kufanya kazi ikiwemo miradi ya ujenzi  kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi ili kuziwezesha zijiongezee kipato na matumizi katika kaya,kuongeza  ujuzi kwa walengwa na kupata miundombinu kwenye jamii.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa TASAF Makao makuu, Alphonce Kyariga aliwataka madiwani na wataalamu wote watakaohusika katika utekelezaji wa mpango huo kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa walengwa ili waweze kutekeleza vyema masharti yote watakayotakiwa kuyatekeleza.

“Moja ya mambo mnayopaswa kuyasimamia ni kuhakikisha fedha yote itakayotolewa katika mpango huu inatumika kama ilivyopangwa, hairuhusiwi kwa halmashauri yoyote ngazi ya wilaya, kata na kijiji kutumia fedha hizi kwa malengo tofauti na kunusuru kaya maskini, watakaokwenda kinyume na maelekezo yake watatakiwa kurejesha fedha hizi,” alieleza Kyariga.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top