Grace Kiwia - Mbunge viti maalumu CHADEMA katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga.

Maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA.
VIONGOZI na wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga wameombwa kuhakikisha wanaheshimu makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu yaliyofikiwa na vyama vilivyoungana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Ombi hilo limetolewa na Naibu Katibu wa Baraza la Umoja wa Wanawake wa CHADEMA Taifa (BAWACHA), Grace Tendega alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Shinyanga katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na chama hicho kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya rasimu ya katiba iliyopendekezwa.

Tendega alisema makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ni halali na yanapaswa kuheshimiwa yakiwa na lengo moja tu ya kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeonesha wazi kushindwa kuwaletea watanzania maendeleo waliyoyatarajia.

Alisema UKAWA kwa hivi sasa ndiyo tumaini la watanzania na kwamba iwapo makubaliano yaliyofikiwa na vyama hivyo yataheshimiwa ni wazi itakuwa rahisi kuing’oa CCM madarakani na kuwawezesha watanzania kupata ukombozi wa mara ya pili kwa lengo la kuboresha maisha yao ili wanufaike na raslimali zilizopo hapa nchini.

“Makubaliano yaliyofikiwa kati ya vyama vya NLD, CUF, NCCR – Mageuzi na CHADEMA ni halali kabisa, na ni lazima tuyatekeleze, msisikilize propaganda za wapinzani wetu kwamba UKAWA hawawezi kuelewana, hizo ni porojo za kutaka kupotosha ukweli, ukweli ni kwamba umoja huu ndiyo pekee wenye uwezo wa kuing’oa CCM madarakani,”

“Ndugu zangu wakazi wa Shinyanga, tumekuja  leo kuzungumza nanyi bila ushabiki wa vyama vyetu vya siasa bali kwa kuzingatia mstakabali wa Taifa letu, maana chini ya utawala wa CCM maisha yetu yanaendelea kuwa magumu kila siku, lazima tuukubali ukweli kwamba CCM inapata jeuri kutokana na ridhaa yenu ninyi wenyewe,” alieleza Tendega.

Akizungumzia kuhusu katiba iliyopendekezwa, Tendega aliwataka wakazi wa Shinyanga kuhakikisha wanapiga kura ya hapana wakati zoezi la upigaji kura za maoni litakapofanyika na kwamba iwapo wataikubali katiba hiyo pendekezwa ni wazi watakuwa wameridhia kwa hiari yao kurejeshwa katika utumwa katika kipindi kingine cha miaka 50.

“Katiba pendekezwa imetupilia mbali maoni yenu, tuhakikishe tunapiga kura ya hapana, vinginevyo tutakuwa tumekubali kuendelea kuwa wateja wa CCM, ni vyema watakapokuja hawa wenzetu wa CCM kunadi katiba yao, hojini ilipo rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba, hii wanayodai ni katiba iliyopendekezwa imejaa maoni ya CCM si ya wananchi,” alieleza.

Naye mwenyekiti wa Taifa wa BAWACHA, Halima Mdee aliwataka wakazi wa mkoa wa Shinyanga kushikamana kwa dhati na kuhakikisha wanakiondosha Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani na kwamba wasitishwe na nguvu ya vyombo vya dola ambavyo hutumika kisiasa zaidi badala ya kuwatumikia watanzania.

“Watanzania umefika wakati muhimu kwetu, tuhakikishe tunashikamana, tuache woga, hata kama CCM watatumia vyombo vya dola kutaka kutudhibiti, lazima tuwe imara, kumbukeni daima hakuna jeshi lolote duniani linaloweza kushindana na nguvu ya umma, tushikamane hali ya nchi yetu ni tete, kila kitu kinauzwa, mwishowe na sisi wenyewe tutauzwa,” alieleza Mdee.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top