Mbunge wa Jimbo la Kishapu, mkoani Shinyanga, Suleiman Nchambi katika moja ya mikutano yake ya kisiasa.
MBUNGE  wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Suleiman Nchambi na diwani wa kata ya Songwa (CCM), Mohamed Shabani kesho Oktoba 27, mwaka huu watawaongoza wakazi wa kijiji cha Maganzo kwenda kufunga lango la kuu la mgodi wa Williamson Diamonds Ltd, uliopo Mwadui wakipinga kitendo cha mauaji dhidi ya wachimbaji wadogo wa madini ya almasi.

Mbali ya kusudio la mbunge huyo pia wakazi wa kijiji cha Maganzo walimkataa mkuu wa kituo kidogo cha Polisi cha Maganzo aliyetajwa kwa jina moja la Oscar kwa kudai hawamtaki na pindi mbunge atakapomaliza mkutano wake aondoke naye kwa vile hana msaada wowote kwa wananchi badala yake huwakumbatia wawekezaji wa mgodi huo wa almasi.

Nchambi alitangaza nia hiyo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Soko la kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ambapo alimuomba diwani wa kata ya Songwa na wakazi wa kijiji cha Maganzo wamuunge mkono ili kufanikisha zoezi hilo.

Akifafanua alisema uamuzi wa kufunga lango la mgodi ni kuzuia kufanyika kwa shughuli zozote baada ya kuchoshwa na vitendo vya mauaji vinavyofanywa na walinzi wa kampuni binafsi inayolinda mgodi huo ambao mara kwa mara huwapiga risasi na kuwaua au kuwasababishia vilema vya maisha wachimbaji wadogo maarufu kwa jina la “Wabeshi.”

Mbunge huyo alisema kwa kipindi kirefu uongozi wa mgodi huo umeshindwa kuheshimu suala la ujirani mwema kwa kuishi vizuri na wananchi waliopo kandokando ya mgodi na kwamba hata kama kuna watu wanaokiuka sheria na kuingia mgodini kwa lengo la kufanya uporaji hukumu yao siyo kuuawa bali ni kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ndugu zangu nimesikia kilio na malalamiko yenu ambayo yametolewa hapa na mwakilishi wenu diwani wetu wa kata ya Songwa, kwa kweli hata mimi ninasikitishwa na taarifa za mara kwa mara za kuuawa vijana wetu wanaotuhumiwa kuingia mgodini kimakosa, hatusemi tunawatetea wahalifu, la hasha, bali tunachokitaka ni sheria kuheshimiwa,”

“Tumejitahidi kutafuta suluhisho la kuwataka wenzetu hawa tukae nao ili tuone jinsi gani tutakavyowasaidia vijana wetu wachimbaji wadogo lakini imeshindikana, kibaya zaidi walinzi wao wameendelea kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga risasi na kuwaua watu wanaotuhumiwa kuingia mgodini kinyume cha sheria, sasa tunasema imetosha,” alieleza Nchambi na kushangiliwa na wananchi.

Alisema kutokana na hali hiyo yeye binafsi kwa kushirikiana na wakazi wote wa kijiji cha Maganzo na vijiji jirani Jumatatu (kesho) atawaongoza wananchi wake akiwemo diwani wa kata ya Songwa kwenda kulifunga lango kuu la mgodi huo kwa lengo kuzuia kufanyika kwa shughuli zozote zile mpaka pale muafaka wa kudumu utakapopatikana.

Nchambi alisema kinachohitajika ni suala la uwepo na amani na utulivu kwa wananchi na kwamba mwekezaji anao wajibu wa kuwaelekeza walinzi wake waache tabia ya kujichukulia sheria mkononi na hata pale watakapowakamata watuhumiwa basi wahakikishe wanafikishwa katika mikono ya vyombo vya dola.

Awali diwani wa kata ya Songwa Mohamed Shabani alimuomba mbunge Nchambi kuingilia kati mgogoro uliodumu kwa kipindi kirefu kati ya wachimbaji wadogo na uongozi wa mgodi huo ambapo walinzi wake huwashambulia mara kwa mara kwa kuwapiga risasi wachimbaji hao wakidai wameingia mgodini kwa lengo la kuiba mchanga wenye madini ya almasi.

“Ndugu mbunge tunakuomba utusaidie kututatulia mgogoro huu maana vinginevyo wachimbaji hawa wadogo watamalizika kwa kupigwa risasi na walinzi wa mgodi wa Williamson, tumejitahidi sana kutafuta utatuzi wa mgogoro huu lakini tumekosa msaada wa viongozi wetu wengine wa kiserikali na hata wa kijiji, sasa tumaini letu limebaki kwako,”

“Kibaya zaidi hata polisi wetu wa kituo kidogo cha Maganzo wamekuwa wameshindwa kuwachukulia hatua zozote walinzi wa mgodi wanaobainika kuwashambulia wachimbaji wadogo kwa kuwapiga risasi, kuna zaidi ya vifo vinane vya wachimbaji hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa,” alieleza Shabani.

Akijibu madai ya kukataliwa kwa mkuu wa kituo kidogo cha polisi, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SSP Longinus Tibishubwamu alikanusha madai ya polisi wa kituo hicho kushirikiana na kampuni ya ulinzi kuwaua wachimbaji wadogo na kwamba yeye binafsi hajapokea rasmi malalamiko dhidi ya vitendo viovu vya mkuu wa kituo hicho.

“Ni kweli kuna matukio mengi ya watu wanaojiita wabeshi kuvamia na kuingia katika mgodi wa Mwadui kinyume cha sheria, lakini mgodi huo haulindwi na polisi, bali kampuni binafsi za ulinzi, hata hivyo tumekuwa tukiwataka wachimbaji wadogo wawe na tabia ya kutii sheria bila shuruti waache vitendo vya uvamizi, vinginevyo wataendelea kujikuta matatani,”

“Jeshi la polisi  kila mara tunatoa elimu hii ya utii wa sheria bila shuruti kwa wenzetu lakini hawatuelewi, na siyo kweli hakuna  hatua tunazochukua dhidi ya walinzi wanaofanya mauaji tunawakamata na kuwafikisha mahakamani, lakini wakati mwingine walinzi huwa wanajihami na kujikuta wakiuua bila kukusudia, hili la mkuu wa kituo halina ukweli wowote, hata hivyo tutalichunguza,” alieleza Tibishubwamu.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top