Mbunge wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora, Dkt. Khamis Kigwangalla. |
Magari, Pikipiki na walinzi wa Jadi maarufu kwa jina la Sungusungu wakiongoza mapokezi ya mbunge wao kuelekea viwanja vya Parking mjini Nzega. |
WAKAZI wa Jimbo la Nzega wamempongeza mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Khamisi Kigwangala kwa uamuzi wake wa kutangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao mwakani na kuahidi kumuunga mkono ili aweze kufanikiwa.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Parking mjini Nzega baada ya mapokezi makubwa wakazi hao walisema kitendo cha Dkt. Kigwangala kutangaza nia mapema ya kutaka kugombea nafasi hiyo kubwa ya kiuongozi nchini kimeonesha wazi jinsi alivyokomaa kiuongozi na kuwaomba watanzania wengine pia wamuunge mkono.
Akisoma risala iliyoandaliwa na wazee wa Nzega mmoja wa wazee hao, Noah Madirisha alisema iwapo wananchi wa Nzega na mkoa wa Tabora kwa ujumla watamuunga mkono mbunge huyo ni wazi ataweza kufanikiwa kuteuliwa kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kinyang’anyiro cha urais mwakani.
Risala hiyo ilieleza kuwa wazee wa Nzega pamoja na wakazi wa jimbo hilo wanatoa pongezi zao za dhati kwa kazi kubwa anayoifanya mbunge huyo katika kuwaletea maendeleo na kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na kwamba kutokana na utendaji wake huo ndiyo maana alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa moja ya kamati za kudumu za bunge.
“Sisi wazee wa Nzega tunatoa pongezi za dhati kutokana na kazi kubwa ambayo umeishatufanyia, mambo mengi ya maendeleo umetekeleza ikiwemo kusaidia wakulima wa zao la pamba na wachimbaji wadogo wa dhahabu, na ndiyo maana hata wabunge wenzako walikuchagua kuwa mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya serikali za mitaa,”
“Kamati hii ni kamati nyeti sana inayohitaji mtu mwenye hekima, serikali za mitaa ni uti wa mgongo wa taifa lolote lile katika dunia hii hivyo huhitaji mtu makini na mwenye hekima kuiongoza, hongera sana kijana wetu, ndani ya utendaji wako umewawezesha wakulima wa pamba kuongeza kilimo chao,”
“Lakini pia kwa miaka hii minne ya utendaji wako umeboresha sekta ya elimu ikiwemo kuanzisha sekondari ya elimu ya juu, kutetea haki za wanyonge kama vile wachimbaji wadogo, hii imekufanya uonekane shujaa wa jimbo letu, imeonesha wewe ni shujaa wetu, mungu akusaidie uendelee kufanikiwa,” ilieleza sehemu ya risala ya wazee.
Pamoja na risala hiyo kwa upande wao viongozi wa walinzi wa jadi (sungusungu) walimtawaza mbunge huyo kuwa mtemi wa Sunsungu na mtemi wa utemi wa Ibambangulu ambapo walimkabidhi silaha mbalimbali za kijadi na kumpa jina la Makaranga Mwanang'washi wakiahidi pia kuwa pamoja nae katika harakati zake za kuwania kiti cha urais hapa nchini.
Akihutubia maelfu ya wananchi hao, Dkt. Kigwangalah aliwapongeza na kuwashukuru kwa mapokezi makubwa ambayo hakuyatarajia ambayo yameonesha dhahiri jinsi gani wanavyomuunga mkono katika utendaji wa kazi zake za kila siku pamoja na kazi ngumu zinazomkabili katika utekelezaji wa majukumu yake.
Hata hivyo mbunge huyo alisema pamoja na pongezi kubwa zilizotolewa kwake lakini bado Tanzania inahitaji viongozi mahiri watakaoweza kuwakomboa watanzania kutoka katika dimbwi la umaskini mkubwa lililowagubika pamoja na nchi yenyewe kuwa na utajiri mkubwa katika kila kona.
“Ndugu wana Nzega wenzangu, waasisi wa taifa hili waliweka misingi ya nchi hii kufanikiwa, waliweka misingi ya Tanzania kutajirika, hili ni fumbo kwa kizazi chetu cha viongozi, waliweka misingi ya kuthamini utu wa kila mmoja wetu, usawa wa kila binadamu na umoja na mshikamano wa kitaifa,”
“Waliweka mfumo wa elimu ulionitoa mimi uswahilini kwetu Musoma road na kunipeleka kwenye ulimwengu wa wasomi kwenye makorido ya vyuo vikuu mashuhuri duniani waliweka mfumo ulionitoa kwenye lindi la umasikini uliokithiri mpaka ulimwengu wa kujenga hoja bungeni na kuota ndoto ya kuwa Rais katika nchi yangu,” alieleza Dkt. Kigwangala.
Dkt. Kigwangala alisema Tanzania hivi sasa inahitaji Rais atakayehakikisha watanzania wanalindwa na mfumo imara wa uchumi wa Taifa kwa kuwaletea maendeleo yatakayowakomboa katika umasikini na kwamba watumishi wote wa umma wanaofanya kazi zao katika mazingira magumu wanastahili kuthaminiwa na kutambuliwa mchango wao.
Kwa upande mwingine mbunge huyo alilazimika kuwatuliza wananchi waliopandwa na jazba wakitaka kuwashambulia baadhi ya vijana waliojitokeza ghafla katika mkutano huo wakiwa na mabango yenye maandishi yaliyomshutumu kwamba ni mmoja wa wabunge mafisadi waliotafuna fedha za umma katika bunge la katiba na kwamba yeye si chaguo la watu wa Nzega.
“Ndugu zangu nakuombeni msibabaishwe wala kutaka kuwaadhibu hawa wenzetu waliokuja na mabango yao, hii ni sehemu ya demokrasia katika nchi yetu, wana haki ya kufikisha ujumbe wao kwa njia yoyote ile wanayoona inafaa, wote ni wapiga kura wangu, naongoza wehu, wagonjwa na hata wasio na akili, niwaombe wao wanione baadae nijibu hoja zao ni haki yao,” alieleza.
Post a Comment