SHERIA NI MSUMENO, LAZIMA ITEKELEZWE. |
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) mkoani Shinyanga kinakusudia kuwaburuza mahakamani baadhi ya waajiri wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wenye tabia ya kukaidi kutekeleza maelekezo ya sheria za kazi nchini.
Mbali ya kuwaburuza mahakamani waajiri hao pia Chama hicho kimesikitishwa na kitendo cha baadhi ya waajiri hao kugoma kushiriki katika mafunzo ya matumizi sahihi ya sheria za kazi yaliyoandaliwa na TUGHE yaliyoandaliwa kwa kuzingatia sheria.
Akizungumza katika semina iliyohusu matumizi sahihi ya sheria za kazi kwa waajiri, wafanyakazi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi mkoani humo, katibu wa TUGHE mkoa wa Shinyanga, Tabu Mambo alisema kitendo cha waajiri wengi kususia mafunzo hayo kimeonesha jinsi gani wasivyothamini baadhi ya sheria za kazi zilizopo.
Mambo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha waajiri, wafanyakazi na viongozi wa vyama wafanyakazi kuzielewa vyema sheria za kazi na jinsi ya matumizi yake pale inapotokea mfanyakazi kwenda kinyume na sheria hizo ambapo alisema iwapo sheria hizo zitaeleweka vizuri zitapunguza migogoro mingi isiyo ya lazima sehemu za kazi.
“Lipo tatizo kubwa kwa baadhi ya waajiri mkoani Shinyanga ambao wamekuwa wakiwaadhibu wafanyakazi bila kuzingatia sheria za kazi zinavyoelekeza, na hii ni pamoja na suala zima la kuruhusu kufanyika kwa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi, baadhi ya waajiri hawayaheshimu, na hudiriki hata kugoma kutoa fedha kwa ajili ya kuendeshea vikao vyake,” alieleza Mambo.
Kwa upande wao washiriki katika semina hiyo mbali ya kusikitishwa na kitendo cha waajiri kushindwa kuhudhuria mafunzo hayo, walimuomba katibu wa TUGHE afanye taratibu za kuwaburuza mahakamani waajiri wote wenye tabia ya kukaidi maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanaokiuka sheria za kazi kwa makusudi.
Aidha walikubaliana kufanyika kwa mafunzo mengine mwakani mwezi Juni, 2015 na kuweka mkazo kwa waajiri wote kushiriki kikamilifu ambapo waliwapongeza Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga, Anselem Tarimo na mkurugenzi wa Mji wa Kahama, Felix Kimario kwa jinsi wanavyoheshimu sheria za kazi ikiwemo kuruhusu kufanyika kwa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi.
Awali katika mada iliyohusu matumizi sahihi ya sheria za kazi iliyowasilishwa na mkurugenzi msaidizi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kutoka makao makuu, Andrew Mwaliwisi alisema wakurugenzi na makatibu tawala wasioheshimu uwepo wa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi wanakiuka sheria na misingi ya utawala bora.
“Inasikitisha kuona watu wenye jukumu la kusimamia sheria ndiyo wanaokuwa mstari wa mbele kutozizingatia, itabidi tuwaarifu makatibu wakuu wa wizara husika waweze kutusaidia tatizo hili, tutakaporudia upya mafunzo haya mwakani waajiri wote waliokwepa waweze kushiriki, ushiriki wa wafanyakazi peke yao bila waajiri hauwezi kumaliza migogoro makazini,” alieleza Mwaliwisi.
Post a Comment