JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga linamsaka mganga mmoja wa jadi anayetuhumiwa kumiliki silaha kinyume cha sheria baada ya kukamata nyumbani kwake bunduki mbili aina ya gobore zikiwa zimefungwa hirizi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alimtaja mganga anayetafutwa kuwa ni Mtabanzila Buyiyi (70) mkazi wa kata ya Malungu wilayani Kahama na kwamba silaha hizo zilikamatwa Oktoba 21, mwaka huu saa 5.41 asubuhi huko nyumbani kwa mganga huyo kata ya Malunga Kahama mjini.
Akifafanua Kamanda Kamugisha alisema siku hiyo ya tukio polisi wakiwa katika doria ya kawaida walipata taarifa kutoka kwa wasiri wao na hivyo kufanya upekuzi katika nyumba ya mganga huyo na kufanikiwa kukamata bunduki hizo mbili zilizokuwa zimefungwa hirizi na kuzungushiwa vipande vya ngozi ya mnyama.
Alisema bunduki zote mbili zilikuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria kutokana na mganga huyo kutokuwa na kibali cha kuzimiliki na inahisiwa huenda zilikuwa zikitumika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu yaliyokuwa yakitokea wilayani Kahama na maeneo mengine ya jirani.
“Juzi Jumanne vijana wetu waliokuwa katika doria ya kawaida walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba mganga huyo humiliki silaha kinyume cha sheria, walikwenda kufanya upekuzi katika nyumba yake na kufanikiwa kukamata silaha hizo ambazo zilikuwa zimefungwa hirizi,”
“Hata hivyo mtuhumiwa huyo aliwahi kutoroka na sasa tunamsaka ili aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la kumiliki silaha kinyume cha sheria za nchi, tunawaomba wananchi watusaidie kwa kutoa taarifa popote watakapomuona ili aweze kukamatwa,” alieleza Kamugisha.
Alisema polisi kwa hivi sasa inamshikilia mtoto wa mganga huyo aliyetajwa kwa jina la Nyamisi Mtabanzila (40) kwa mahojiano zaidi ili kuweza kubaini sababu ya yeye na baba yake kufanya kazi ya uganga bila leseni inayowaruhusu kutoa huduma hiyo huku wakimiliki silaha kinyume cha sheria.
Post a Comment