Acheni kubeza kazi za mbunge, mpeni ushirikiano.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja akiteta jambo na mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini na Naibu Waziri wa Nishati na Madini nchini, Stephen Masele.

WAKAZI wa Jimbo la Shinyanga mjini wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kuacha kubeza kazi zinazotekelezwa na mbunge wa Jimbo hilo, Stephen Masele na badala yake wamuunge mkono ili aweze kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Ushauri huo umetolewa  na mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alipokuwa akiwahutubia wakazi wa manispaa na wageni kutoka nje ya mkoa wa Shinyanga kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya wajawazito katika kituo cha afya cha Kambarage manispaa ya Shinyanga lengo likiwa kukusanya shilingi milioni 105.

Katika hotuba yake Mgeja alielezea kushangazwa na baadhi ya wananchi wakiwemo wanachama wa CCM wanaobeza shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazotekelezwa na mbunge wao na kwamba kitendo wanachokifanya kinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokufanikiwa kwa mipango mbalimbali ya kimaendeleo katika jimbo hilo.

Alisema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na mbunge huyo ambaye pia ni Naibu waziri wa Nishati na madini nchini lakini bado wapo watu wanaobeza kazi anazozifanya kutokana na chuki binafsi walizonazo dhidi yake na kwamba maendeleo anayotekeleza ni ya wananchi wote bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa, dini au kabila.

“Ndugu zangu watu wa Shinyanga, leo hii lazima tuelezane ukweli, tufike sehemu tukubali yaishe, kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiwaeleza umuhimu wa Masele (Stephen) hamkuwa mkiamini, na baadhi yenu mliendelea kuona hakuna anachokifanya, lakini leo ukweli umedhihirika hapa kutoka kwa watu wa nje ya mkoa wetu wa Shinyanga,”

“Hawa wageni wetu tuliowakaribisha katika harambee hii wamethibitisha Masele ni lulu ya Taifa, kwa hali hii basi wale wote wenye vinyongo, chuki na roho za korosho dhidi yake wanapaswa kuviondoa mioyoni mwao na tumuunge mkono aweze kutekeleza vyema ilani yetu ya uchaguzi ya CCM, badala ya kumpiga vita,” alieleza Mgeja.

Mgeja alisema si kila kiongozi ni mwanasiasa na si kila mwanasiasa ni kiongozi, lakini kwa Masele amebahatika kupata sifa zote mbili, na kwamba ni nadra sana kumpata mtu mwenye sifa zote hizo, maana wapo wengi wanaoonekana wakijiita wanasiasa kumbe siyo bali ni wanaharakati wa kupiga kelele tu majukwaani. 

Kwa upande mwingine Mgeja alimpongeza diwani wa kata ya Kambarage Nyangaki Shilungushela (CHADEMA) kwa jinsi alivyoshirikiana na wananchi wa kata yake katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha afya bila kujali kwamba anatokana na chama cha upinzani na kwamba maendeleo yatakayopatikana hayatachagua mtu kwa itikadi ya chama chake cha siasa.

Katika harambee hiyo iliyowashirikisha pia wakuu wa wilaya kutoka Igunga, Iramba, Tarime, Bukombe na Bunda iliyoandaliwa na mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini Stephen Masele, jumla ya shilingi milioni 115 zilipatikana ikiwemo mifuko 690 ya saruji ambapo mbunge huyo na rafiki zake walichangia shilingi milioni 45 taslimu.

Kwa upande wao wageni mbalimbali waliopata fursa ya kuzungumza katika harambee hiyo walielezea jinsi wanavyothamini mchango wa Naibu waziri Masele hasa kwa jinsi alivyoweza kupunguza migogoro ya muda mrefu kati ya wachimbaji wadogo wa madini na wawekezaji kutoka nje na hivi sasa wengi wao wana leseni halali za kufanya kazi hiyo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top