Mmoja wa watu wanaodaiwa kugeuzwa Msukule (wa tatu kutoka kushoto) aliyekamatwa katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji cha Itilima wilaya ya Shinyanga. Hata hivyo baadae ilibainika alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa akili.

Kijana aliyehisiwa kuwa ni Msukule akiwa ndani ya gari la Polisi tayari kwa kupelekwa kituoni.  Hata hivyo hapakuwa na ukweli wowote kuhusiana na madai ya wakazi wa kijiji cha Itilima kwamba kijana huyo ni Msukule.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga kimeshitushwa na taarifa za kuibuka kwa kundi la waganga wa jadi maarufu kwa jina la “Lambalamba” au “Kamchape” wanaopita vijijini wakiwachangisha wananchi fedha kwa nguvu wakidai ni malipo ya kazi ya kuwafichua wachawi katika maeneo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alisema kuzuka kwa kundi hilo kunaweza kusababisha kuendelea kwa matukio ya mauaji ya kikatili dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi kutokana na imani za kishirikina.

Mgeja alisema ni muhimu kwa viongozi wa serikali mkoani humo wahakikishe wanawasaka na kuwakamata wafuasi wa kundi hilo ambalo tayari limesababisha matatizo kwa wakazi wa Shinyanga vijijini huku baadhi yao wakinyang’anywa kwa nguvu mifugo na fedha zao na kwamba serikali ya CCM haipaswi kufumbia macho vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya mwenyekiti huyo wa CCM kwa ajili ya kukagua utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, kundi hilo linadaiwa kuingia vijijini likiwalazimisha wanavijiji kutoa fedha ili wafichuliwe wachawi na watu wanaofuga ‘misukule.’

Akifafanua mkuu huyo wa wilaya alisema watu hao wamekuwa wakilazimisha wanavijiji kila kaya kutoa shilingi 5,000 kama gharama za kuwasaka wachawi katika vijiji vyao pamoja na kuwarejesha watu waliogeuzwa na wachawi misukule hali ambayo imesababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa wananchi.

“Mheshimiwa mwenyekiti hawa watu wanadai wana uwezo mkubwa wa kuywafichua wachawi, kurejesha watu waliogeuzwa misukule na wale wanaouzia mvua kunyesha, hili limetushitua watendaji wa serikali maana linaweza kuchangia zaidi matukio ya mauaji kutokana na watu kuamua kulipizana visasi,”

“Tumeelezwa kwamba watu hawa wamekuwa wakiwasumbua sana wananchi, wengi wamelazimishwa kutoa ng’ombe au mbuzi baada ya kudaiwa kuwa ni wachawi, hata hivyo kila kaya inachangishwa shilingi 5,000 kama gharama za kufanyika kwa kazi hiyo, na kibaya zaidi wanasaidiwa na baadhi ya watendaji wetu wa serikali,” alieleza Nyamubi.

Nyamubi alisema tayari lambalamba wanne wamekamatwa (majina yamehifadhiwa) na kwamba katika mahojiano ya awali walionesha kupewa vibali na mtumishi mmoja wa manispaa ambaye pia ameagiza akamatwe na kuwekwa ndani hata hivyo kazi hiyo waliifanya Shinyanga.

“Binafsi nilisikitishwa na kitendo kilichofanywa na mtendaji huyo wa serikali kutoa vibali kwa watu hawa, na nilishituka zaidi aliponieleza kwa mwaka uliopita ametoa vibali kwa waganga wa jadi 100, niliagiza akamatwe na kuwekwa ndani, maana ni mmoja wa watu wanaochangia kuongezeka kwa tatizo,” alieleza Nyamubi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top