Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga Khamis Mgeja, akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya agizo la CCM kwa viongozi na watendaji wa Serikali mkoani humo kuhakikisha wanakomesha vitendo vya mauaji ya kikatili dhidi ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi na ubakwaji wa watoto.

Dc Nyamubi akitoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika shule ya msingi Buhangija Jumuishi manispaa ya Shinyanga uliotolewa na wanachama wa vikundi vya VIKOBA vilivyopo chini ya YWCA Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi akizungumza na mmoja wa watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaotunzwa katika shule ya msingi Buhangija Jumuishi ambapo alimthibitishia kwamba serikali itaendelea kuwahakikisha usalama wao ili waweze kuishi kama watu wengine wasio na ulemavu wa ngozi
KUFUATIA kuibuka upya kwa mauaji ya kikatili dhidi ya vikongwe na ubakwaji wa watoto wadogo ambao pia hutobolewa macho, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga kimetoa agizo kwa viongozi na watendaji wote wa serikali mkoani humo kuchukua hatua mara moja  za kukabiliana na wimbi la matukio hayo yanayochafua sifa ya mkoa.

Agizo hilo limetolewa na mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa serikali, halmashauri ya manispaa ya Shinyanga na baadhi ya madiwani katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili wilayani Shinyanga kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015.

Mgeja alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi akielezea tukio la kikatili lililotokea wiki mbili zilizopita ambapo mtoto mwenye umri wa miaka tisa mkazi wa kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga alibakwa hadi kufa  na watu wasiojulikana kisha alitobolewa macho yake yote mawili.

Pia ilielezwa kuwepo kwa ongezeko la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe katika siku za hivi karibuni mkoani humo hali ambayo imesababisha wakazi wake wengi wakiwemo wazazi na walezi wenye watoto wa kike kuishi maisha ya wasiwasi wakihofia maisha ya wazee na watoto wao.

Takwimu za kipolisi zinaonesha kati ya Januari hadi Desemba, 2013 matukio ya mauaji ya vikongwe yaliyoripotiwa mkoani Shinyanga yalikuwa ni 53 ambapo matukio 25 yakitokea wilayani Kahama na katika kipindi cha miezi minne Januari hadi Aprili 30 yameripotiwa matukio 19 kati yake 14 yakitokea katika wilaya Kahama.

Mgeja alisema kuanzia sasa viongozi na watendaji wa serikali na halmashauri za wilaya waweke mikakati madhubuti itakayokuwa endelevu ya jinsi ya kukabiliana na matukio hayo kwa kuhakikisha hayatokei badala ya kusubiri kuyashughulikia baada ya kutokea hali ambayo aliifafanisha na kitendo cha zimamoto.

“CCM tumesikitishwa sana na taarifa ya tukio la kuuawa kikatili kwa mtoto aliyebakwa na mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu yanayoonekana kurejea upya katika mkoa wetu, kwa kweli yanachafua sifa ya mkoa wetu,”

“Kuanzia sasa tunawaagiza viongozi na watendaji wote wa serikali na wenzetu wa halmashauri za wilaya anzeni kuweka mikakati ya kukomesha mauaji na vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani mwetu, acheni tabia ya kukaa na kusubiri kushughulikia matukio yanapotokea,”

“Suala la ulinzi na usalama limo ndani ya ilani yetu ya uchaguzi, hivyo ni muhimu wenzetu ambao ndiyo watekelezaji wa ilani hiyo muhakikishe wananchi wanalindwa na wanaishi kwa amani na utulivu kama ilivyoelezwa ndani ya ibara ya 206 hadi 208 kuhusu ulinzi kwa makundi maalumu,” alieleza Mgeja.

Kwa upande mwingine Mgeja amewaomba wakazi wa mkoa wa Shinyanga kushirikiana na viongozi na watendaji wa serikali kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili badala ya kuliacha jukumu hilo mikononi mwa vyombo vya dola pekee na kwamba kila mwananchi ni mlinzi katika eneo analoishi hivyo ni rahisi zaidi kwa kuwatambua wale wote wanaojihusisha na ukatili huo wa kinyama.

“Naamini tukiweka mikakati endelevu katika ngazi zote, mkoa, wilaya, kata hadi vijijini na tuwe na agenda ya kudumu katika vikao vyetu tujadiliane jinsi ya kupamba na janga hili ambalo ni janga la mkoa, tusiwe na tabia ya kushughulikia matatizo haya kwa mfano wa zimamoto, yaani tunakaa tukisubiri yatokee ndipo tunaanza kuhangaika, hapana tuache mtindo huu,” alieleza.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top