Nipo tayari kwa kuonesha vimbwaga - Ndivyo inavyoelekea nyoka huyu aina ya Sawaka akieleza. |
Wasanii wakijiandaa kutoa nyoka ili kuserebuka nao. |
Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Shinyanga mjini, Msetti mwenye mwili wenye mawasiliano mazuri na meza akifuatilia mkutano kwa umakini mkubwa. |
Wasanii wa ngoma ya kucheza na nyoka maarufu kwa jina la Wagoyangi wakifanya vitu vyao muda mfupi kabla ya mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Ngokolo mitumbani, manispaa ya Shinyanga. |
HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani
Shinyanga kimekanusha tuhuma zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) zikiwatuhumu baadhi ya makada wake kudaiwa kupanga njama za kutaka
kumuua katibu mkuu wake, Dkt. Wilbroad Slaa na kudai waliotoa tuhuma hizo
wamefilisika kisiasa.
Tuhuma hizo zilizotolewa na madiwani wawili
waliorejea CHADEMA, Zacharia Mfuko aliyekuwa diwani wa kata ya Masekelo na
Sebastian Peter wa kata ya Ngokolo waliodai mbunge wa Shinyanga mjini Stephen
Masele na viongozi wa CCM walipanga kulipua helkopta iliyokuwa imembeba Dkt.
Slaa ikiwa ziarani Shinyanga.
Madiwani hao ambao awali walitangaza mbele ya
mkutano wa hadhara kukihama kwa hiari chama chao cha CHADEMA na kujiunga na CCM
na baadae kuamua kurejea tena CHADEMA wakidai kutokulipwa fedha walizoahidiwa
na viongozi wa CCM iwapo wangekihama chama chao walitoa tuhuma hizo nzito mbele
ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Wakihutubia kwenye mikutano ya hadhara
iliyofanyika katika kata za Masekelo na Ngokolo mwenyekiti wa CCM mkoani
Shinyanga, Khamis Mgeja, mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini Stephen Masele na
mbunge wa Jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi walikanusha tuhuma hizo na kudai
zimetolewa na waganga njaa na watu waliofilisika kisiasa.
Kwa upande wake mbunge Masele ambaye pia ni
Naibu waziri wa Nishati na Madini akikakanusha madai hayo mbali ya kushangazwa
na tuhuma hizo alisema hana muda wa kubishana na madiwani hao kutokana na
uzushi waliouzusha na kwamba hana sababu ya kutaka kumuua Dkt. Slaa kwa vile
hana muda wa kuhangaika naye.
Alisema haiwezi kutokea hata siku moja Dkt.
Slaa akagombea ubunge katika jimbo la Shinyanga mjini na kwamba watu waliotoa
madai ya kwamba alipanga kuilipua helkopta aliyokuwa ameipata ni uongo uliovuka
mipaka kwa vile siasa hata siku moja si kuuana bali ni kushindana kwa nguvu za
hoja.
“Naomba nitumie mkutano huu kukanusha yale yote
yaliyosemwa na watu wa CHADEMA kwamba nilitaka kutungua helkopta waliyokuwa
wamepanda Dkt. Slaa na Mnyika, siyo kweli, sina muda wala sijashiriki wala
sintokaa nishiriki mipango michafu ambayo haina kichwa wala miguu ni upuuzi
kabisa kudai nahangaika na Dkt. Slaa,”
“Hata hivyo niwakumbushe kitu kimoja juu ya
hawa watu, walipotoka CHADEMA kuja CCM walisema, Masele alikuwa anawindwa kama
swala ili auawe na kumwagiwa tindikali, pia katika uwanja uleule walidai marehemu
Philipo Shelembi aliuawa kwa mipango ya viongozi wa CHADEMA, leo vipi wageuke
na kudai CCM tulitaka kumuua Dkt. Slaa,” alihoji. Masele.
Alisema yeye akiwa mbunge wa Jimbo la Shinyanga
mjini na Naibu waziri wa wizara ya Nishati na Madini nchini hana muda wa
kupoteza kwa kubishana na vijana hao wawili
katika mambo yasiyo na maslahi kwa wakazi wa jimbo lake.
Alisema
muda alionao hivi sasa ni wa kuwahangaikia wapiga kura wake wa Jimbo la
Shinyanga mjini katika kuwaletea maendeleo aliyowaahidi mwaka 2010 na tayari
ameishatekeleza sehemu kubwa ya ahadi hizo ikiwemo kufikisha maji katika vijiji
vyote vilivyo kandokando ya manispaa ya Shinyanga.
Masele aliwahakikishia wakazi wa Shinyanga
kwamba atahakikisha ahadi zake zote alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi
anatekeleza zote na hii ni kutokana na nafasi aliyopewa na mtukufu Rais Jakaya
Kikwete ya kuwa Naibu waziri na hivyo kupata fursa ya kufuatilia kwa ukaribu
zaidi mambo mengi ya kimaendeleo katika
jimbo lake.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis
Mgeja aliwataka wana CCM kutohangaishwa na porojo zinazotolewa na madiwani hao
wawili na kwamba kauli zao hizo zimelenga kutaka kuwahamisha kwenye agenda ya
utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ili pasiwepo mafanikio yaliyotarajiwa.
“Ndugu zangu CCM haina muda wa kuhangaika na
watu kutoka vyama vya upinzani, kama ni timu basi timu yetu imekamilika kila
eneo, kuanzia mwenyekiti wake wa Taifa hadi ngazi ya chini tupo kamili, hawa
wanaotua tuhuma hizi dhidi ya makada wetu ni vinyonga wa kisiasa, ni waganga
njaa, msipoteze muda kuwasikiliza,”
“Tuwe makini wasituhamishe kwenye agenda yetu,
cha muhimu tuongeze mshikamano wetu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, tusirudie makosa
tuliyoyafanya mwaka 2009 na 2010, tujipange vyema, na CCM inaamini arobaini ya
CHADEMA imekaribia, watarudi kwenye biashara ya rejareja,” alieleza Mgeja.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi
aliwataka wana CCM wa Shinyanga kuhakikisha hawafanyi makosa katika uchaguzi
mkuu ujao kwa kuepuka kuchagua wagombea kutoka vyama vya upinzani ambao
wameonesha wazi hawana msimamo wala mpango wa kuwasaidia watanzania.
Alimpongeza Masele kwa kazi kubwa alizozifanya
katika jimbo lake kwa kipindi cha miaka minne iliyopita akitoa mfano wa ujenzi
wa viwanda vikubwa vya kusindika ngozi, nyuzi na kutengeneza mafuta ya kula
ambavyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira
miongoni mwa vijana wa jimbo la Shinyanga mjini.
Post a Comment