Kaimu Mwenyekiti wa Taifa  wa Chama cha  Alliance for Change and Transparance Tanzania (ACT)  Lucas Limbu akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mahakama ya mwanzo manispaa ya Shinyanga ukiwa ni mkutano wao wa kwanza kanda ya ziwa.

Hapa Kaimu mwenyekiti wa Taifa wa ACT- Tanzania, Lucas Limbu akigawa bure kadi za chama hicho kwa baadhi ya wananchi wachache waliohudhuria mkutano wake wa hadhara.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparance Tanzania (ACT) kimejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupata wasikilizaji wachache katika mkutano wake wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya kukitambulisha rasmi mkoani Shinyanga.

Hali hiyo ilikuwa ni tofauti na matarajio ya watu wengi kutokana na taarifa za awali kwamba chama hicho hivi sasa kinakubalika na watanzania wengi na tayari kina idadi kubwa ya wanachama huku kikitoa wito kwa wananchi wajiunge kwa wingi kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa hapa nchini.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini Shinyanga Kaimu mwenyekiti wa Taifa wa ACT Lucas Limbu alisema lengo la kuanzishwa kwa chama chake ni kutaka kuwakomboa watanzania ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi katika maisha ya tabu.

Limbu alisema pamoja na baadhi ya watu kuitangaza vibaya ACT kuwa ni Tawi la Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini ukweli utabaki palepale kwamba ni chama cha upinzani chenye lengo la kutaka kukamata dola ili kuweza kuwaletea maisha mazuri watanzania tofauti na hivi sasa ambapo uchumi wa watanzania wengi hauridhishi.

“Ndugu zangu leo tupo hapa katika mji wenu wa Shinyanga kwa lengo la kukitangaza chama chetu, hiki ni chama cha upinzani halisi kama vilivyo vyama vingine vya upinzani na siyo kweli kwamba ni Tawi la CCM, huu ni upuuzi, tunaomba muwapuuze watu hawa, ACT ni chama halisi cha upinzani hapa nchini,”

“Hawa wanaodai sisi ni Tawi la CCM wana lengo la kutaka kufifisha juhudi zetu na kusababisha tukose wanachama wa kutosha, tunakuombeni mpuuze porojo hizo na mjiunge kwa wingi na ACT chama imara na mbadala wa vyama vilivyopo vya upinzani kwa sasa, tunaomba mtuunge mkono,” alieleza Limbu.

Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Athuman Khalfan alisema hivi sasa ACT kimeanza kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kukitangaza kwa wananchi na kutafuta wanachama ambapo kwa mikoa ya kanda ya Ziwa kitatembelea mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita, Mwanza na Mara.

Khalfan alisema ACT ina lengo zuri kwa watanzania na kwamba kitahakikisha kinafuata na kuenzi sera za Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ndiye muasisi wa taifa hili kwa vile daima alikuwa akisimamia haki na kutanguliza mbele suala la utaifa.

Kwa upande mwingine mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho aliwataka wakazi wa mkoa wa Shinyanga kuwapuuza wale wote wanaopanda majukwaani na kupiga kelele wakidai CCM haijafanya jambo lolote la maana hapa nchini na kwamba hizo ni siasa zilizopitwa na wakati kwa vile kuna mambo mazuri ambayo CCM imeyafanya.

Hata hivyo baada ya mkutano huo wa hadhara viongozi wa chama hicho waligawa bure kadi za chama chao kwa wananchi wachache waliokuwa wamehudhuria huku wakiahidi kurejea tena mkoani humo kwa lengo la kuwapokea viongozi mbalimbali kutoka vyama vingine vya siasa watakaojiunga na ACT pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wake.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top