Shinyanga
WAKAZI
wa Mkoa wa Shinyanga wameshauriwa kutopatwa na hofu yoyote juu ya ugonjwa
hatari wa Ebola na kwamba mpaka hivi sasa hakuna taarifa zozote za kuwepo kwa
ugonjwa huo hapa nchini.
Mbali ya kuondolewa hofu hiyo pia wameshauriwa
kupuuza taarifa zinazosambazwa na baadhi
ya watu wakidai ugonjwa huo unaweza kuingia nchini wakati wowote baada ya
kupatikana kwa mtu mmoja nchini Rwanda anayehisiwa kuwa na Ebola.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,
mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Ntuli Kapologwe alisema mpaka hivi sasa
hakuna taarifa zozote za kuwepo kwa ugonjwa huo nchini na kwamba hata kama
utabainika kuingia nchini anayepaswa kutoa taarifa kitaifa ni Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii.
Dkt. Kapologwe alisema wapo baadhi ya watu
wamekuwa wakisambaza taarifa zinazowatia hofu wananchi na kwamba katika ngazi
ya mkoa mtu anayestahili kutoa taarifa ya kuwepo ugonjwa huo ni mganga mkuu wa
mkoa ambaye ndiye mtaalamu katika masuala yote ya kiafya mkoani.
“Mpaka sasa hakuna taarifa za kuwepo kwa
ugonjwa huu, hivyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi, badala yake waendelee
kufanya kazi zao bila ya hofu yoyote, na iwapo itabainika kuna mtu mwenye
ugonjwa huo, basi wizara ya afya au waganga wa mikoa ndiyo wenye wajibu wa
kutoa taarifa mara moja,” alisema.
Alisema tayari yeye na timu ya wataalamu
wenzake mkoani humo wamekaa na kujipanga ili pale patakapotokea mtu ye yote
atakayehisiwa kuwa na ugonjwa huo, timu hiyo iweze kwenda mara moja sehemu
alipo mgonjwa huyo kwa lengo la kumchunguza kwa kina ili kujiridhisha kabla ya
kutangaza kuwa ana ugonjwa wa Ebola.
“Tumejiandaa kikamilifu katika kukabiliana na
ugonjwa huu iwapo itatokea umeingia mkoani kwetu, tayari tumeisha nunua vifaa
tiba na vizuizi vya ugonjwa huo na pia vifaa vilivyoagizwa na serikali viko
njiani tunatarajia kuvipokea wakati wowote kuanzia sasa,”
“Tunachowaomba wananchi popote pale walipo watakapomuona mtu
ye yote anayeonesha dalili za kuwa na ugonjwa usio wa kawaida wamuwahishe
hospitali mara moja badala ya kutafuta tiba mbadala za mitaani au kumpeleka kwa
waganga wa kienyeji,”
“Ni muhimu kwanza wakazielewa dalili za ugonjwa
huu ambazo ni mgonjwa kuwa na homa kali huku akitokwa na damu sehemu zote za
wazi katika mwili wake, hivyo mtu akiwa na dalili hizo ni muhimu awahishwe
hospitali bila ya kucheleweshwa,” alieleza Dkt. Kapologwe.
Post a Comment