Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha amemtaja mganga huyo wa jadi kuwa ni Mihayo Isheli mkazi wa kijiji cha Buduba kata ya Nyandekwa wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga na kwamba tukio hilo lililitokea huko kijijini Buduba.
Akifafanua Kamanda Kamugisha alisema siku hiyo ya tukio Kawawa akiwa nyumbani kwa mganga huyo akisubiri kupatiwa matibabu ghafla alichanganyikiwa na kuanza kufanya fujo ambapo aliamua kumshambulia kwa kipigo mganga wake hali iliyosababisha mganga pia achukue hatua za kujihami huku akisaidiwa na wagonjwa wengine.
“Huyu mgonjwa akiwa anasubiri matibabu kichaa chake kilipanda ghafla na hivyo alianza kumshambulia kwa kipigo mganga aliyekuwa akimtibu, mganga naye katika kujihami akisaidiwa na wagonjwa wengine aliamua kujibu mapigo ambapo alichukua kitu kizito na kumpiga nacho kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo,”
“Hata hivyo baada ya kubaini mteja wake amekufa mganga pamoja na familia yake na wagonjwa wengine waliokuwa wakitibiwa walitoroka na kwenda kusikojulikana na hivi sasa tunaendelea na msako wa kumtafuta popote alipo ili aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji,” alieleza Kamugisha.
Katika tukio lingine mkazi wa kijiji cha Ilamba kata ya Igwamanoni wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, Masumbuko Ramadhani (30) ameuawa kikatili baada ya kushambuliwa kwa kipigo cha fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na wananchi wenye hasira akituhumiwa kwa kosa la wizi wa baiskeli ya binamu yake Mhoja Ramadhani.
Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea huko katika kijiji cha Ilamba wilayani Kahama ambapo hata hivyo mmiliki wa baiskeli iliyodaiwa kuibwa, Mhoja Ramadhani alitoweka katika eneo la tukio baada ya kubaini binamu yake ameuawa.
Hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea na uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini chanzo chake ambapo imerudia kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa vile mara nyingi watu wanaouawa baada ya kupigiwa yowe wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali huwa siyo wahusika halisi.
Post a Comment