WATU saba wamekufa katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Shinyanga akiwemo mkazi wa kijiji Shunu wilayani Kahama aliyegongwa na trekta wakati akitembea kando ya barabara ya Kahama – Masumbwe wilayani Bukombe mkoa wa Geita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha amemtaja mtu aliyegongwa na trekta na kufa papo hapo kuwa ni Esther Marco mwenye umri wa kati ya miaka 28 na 29 na kwamba ajali  hiyo ilitokea juzi saa 12.30 jioni.

Hata hivyo Kamanda Kamugisha alisema dreva aliyekuwa akiendesha trekta lililomgonga mwananchi huyo hakusimama mara baada ya ajali hiyo na hivyo kutokuwa rahisi kutambulika namba za usajili wake wala aina ya trekta lenyewe na hivi sasa polisi inaendelea na uchunguzi ili kuweza kumbaini.

Katika tukio la pili utingo mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Rashid Juma amekufa papo baada ya kuanguka gari Scania namba T.214 AGV lililokuwa limebeba marobota ya pamba kuacha njia ya kupinduka katika barabara ya Nindo – Shinyanga.

Kamanda Kamugisha alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 2.40 asubuhi wakati gari hilo mali ya Kampuni Afrisian Ginnery lililokuwa likiendeshwa na dereva  Justine Philemon (35) mkazi wa Majengo manispaa ya Shinyanga likisafirisha pamba kwenda kiwandani ambapo pia watu wanne walijeruhiwa.

Majeruhi katika ajali hiyo walitajwa kuwa Charles Peter (19) mkazi wa Kolandoto, Daniel James (18), Philipo Charles (19) na Richard Samwel (19) wote wakazi wa Ibadakuli manispaa ya Shinyanga ambao wamelazwa katika hospitali ya serikali wakipatiwa matibabu na hali zao zimetajwa kuendelea vizuri.

Kamanda Kamugisha alisema polisi hivi inamtafuta dereva wa gari hilo aliyetoroka baada ya ajali ambapo uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

Mtu wa tatu aliyekufa alitajwa kuwa ni mkazi wa kitongoji cha Igembesabo kijiji cha Mpumbula wilayani Kishapu, Moto Bangili (40) alikutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani juu ya dari la nyumba aliyokuwa akiishi yeye na mkewe Astelia John.

Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea Agosti 4, mwaka huu saa 12 jioni na kwamba mkewe ndiye aliyeugundua mwili wa mumewe ukiwa unaning’inia juu ya dari na kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali huku ikihisiwa chanzo cha marehemu kuchukua uamuzi huo ni kutokana na kuugua kipindi kirefu ugonjwa wa kiuno na tumbo.

Huko katika kijiji cha Mwakitolyo wilayani Shinyanga watu wawili walikufa wakiwa ndani ya shimo walipokuwa wakichimba udongo unaohisiwa kuwa na madini ya dhahabu kutokana na kukosa hewa walipokuwa wakiendelea na shughuli zao ndani ya shimo hilo.

Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita saa tisa mchana na kuwataja waliokufa kuwa ni Simba Mayeka (55) na Limwa Buguruti (35) wote wakazi wa kijiji cha Mwakitolyo wilayani Shinyanga.

Mtu wa sita aliyekufa alitajwa kwa jina la Michael Jilige (70) mkazi wa kijiji cha Lyabukande wilayani Shinyanga aliyegongwa na gari na kufa papo hapo alipokuwa akiendesha baiskeli kandokando na barabara ya Salawe – Shinyanga.

Kamanda Kamugisha alisema ajali hiyo ilitokea Agosti 4, mwaka huu saa 12.30 asubuhi ambapo mwananchi huyo aligongwa na gari aina ya Fuso lenye namba T.926 AXR likiendeshwa na dereva Stadius Paulo (25) aliyekuwa akiendesha gari lake kwa mwendo wa kasi.na hivi sasa anasakwa na polisi ili aweze kukamatwa.

Katika tukio lingine lililotokea huko katika kijiji na kata ya Ngogwa wilayani Kahama, mkazi wa kijiji hicho aliyetambuliwa kwa jina la Edward Deogratius (20) alikutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani na mwili wake ukining’inia juu ya mti jirani na nyumba ya baba yake Deogratius Sita.

Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo wapiti njia waliugundua mwili wake saa 4.00 usiku na kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya kijiji. Hata hivyo haikufahamika mara moja chanzo cha yeye kuchukua uamuzi huo kutokana na kutokuacha ujumbe wowote.

Mwisho
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top