Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA Taifa, Wilfred Lwakatare akifafanua kuhusu rasimu ya katiba ambayo ndiyo inayopaswa kujadiliwa na wabunge wa Bunge maalumu la katiba. (BMK). |
Viongozi mbalimbali wa CHADEMA wakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Taifa wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga. |
Sehemu ya wakazi wa Shinyanga wakifuatilia mkutano wa CHADEMA. |
Red Bridged wakihakikisha usalama unakuwepo mkutanoni wakati wote. |
CHAMA Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kimesisitiza kwamba wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) hawatarejea ndani ya bunge maalumu la katiba (BMK) mpaka pale Chama cha
Mapinduzi (CCM) kitakapokubali kujadili rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Mbali ya kusisitiza kutorejea bungeni kwa wajumbe wa UKAWA chama hicho kimetoa wito kwa vijana wote na watu wengine nchini ambao hawajaandikishwa ndani ya daftari la wapiga kura kujitokeza kwa wingi pale kazi ya uboreshaji wa daftari hilo itakapoanza.
Wito huo umetolewa mjini Shinyanga na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA Taifa, Wilfred Lwakatare alipokuwa akiwahutubia wakazi wa mji huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo kwa lengo la kuwafafanulia wananchi sababu zinazowazuia UKAWA kurejea bungeni.
Lwakatare alisema pamoja na baadhi ya wananchi kuwalaumu wajumbe wa UKAWA kwamba kitendo chao cha kugoma kurejea bungeni kinaweza kusababisha kutopatikana kwa katiba mpya hapa nchini, hata hivyo msimamo wao mpaka hivi sasa ni huohuo mpaka pale CCM watakapokubali kujadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Alisema hata kama CCM watashinikiza kwa kutumia mbinu chafu,mabavu na wingi wao bungeni kupitisha rasimu yao yenye muundo wa serikali mbili bado watanzania kwa umoja wao watapiga kura za kuikataa na kwamba watanzania wa leo siyo wa mwaka 47 waliokuwa wakikubali kuburuzwa katika kila jambo bila kujali mstakabali wa maisha yao ya baadae.
“Ndugu zangu msibabaishwe na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wakiongozwa na watu wa CCM kwamba UKAWA hawakutenda haki kwa kitendo chao cha kususia bunge maalumu la katiba, na kwamba wanaweza kusababisha kutopatikana kwa katiba mpya, ukweli ni kwamba hawakuwa wendawazimu, hawako tayari kujadili rasimu ya CCM,”
“Kinachopiganiwa na UKAWA ni kutetea maoni ya watanzania waliopoteza muda wao mwingi kwenda mbele ya Tume ya Jaji Joseph Warioba kutoa maoni yao kuhusiana na muundo upi wa katiba mpya wanaoutaka hivi sasa, lakini ajabu wenzetu wa CCM wanataka kuyaweka pembeni maoni hayo na kujadili ya kwao yenye maslahi yao binafsi,” alieleza Lwakatare.
Kwa upande mwingine Lwakatare alisema moja ya sababu inayosababisha CCM wakatae kujadili rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba ni rasimu hiyo kuainisha mambo muhimu yaliyopendekezwa na wananchi kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote ambayo yatawanyima fursa wao (CCM) kujinufaisha.
Alisema baadhi ya vifungu vilivyopendekezwa ndani ya rasimu ya Tume ya Jaji Warioba vinaondoa mianya ya watu kufanya ufisadi wa mali ya umma kama jinsi ilivyoelezwa katika ibara ya 19 ya rasimu hiyo inayozungumzia matumizi ya mali ya umma na ile ya 20 ikihusu utekelezaji wa masharti ya maadili.
“Naomba msikubali kudanganywa, UKAWA wako makini sana katika kuhakikisha maoni yenu mliyoyatoa mbele ya Tume ya Jaji Warioba yanaheshimiwa, hawa CCM ni wa watu wa ajabu sana hata mambo ya msingi wao wanayapinga, mfano ni ibara za 19 na 20 wanataka vifungu hivyo vifutwe, someni vizuri rasimu hiyo muielewe msidanganywe,”
“Ibara hiyo ya 19 inazungumzia, naomba niwasomee; “….kiongozi wa umma hatoruhusiwa kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo zilizokodishwa kwa serikali, kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi au kumpatia mtu mwingine manufaa yoyote, hili CCM hawataki liwemo,” alieleza Lwakatare.
Kutokana na hali hiyo alisema hivi sasa vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF vitaendesha mikutano kwa nchi nzima kuwaelimisha watanzania na iwapo CCM watashinikiza kupitisha rasimu ya katiba wanayoitaka wao wananchi waweze kupiga kura nyingi za hapana bila woga kwa kuikataa rasimu hiyo.
Post a Comment