Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka akitoa maelekezo kwa baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa katika mafunzo hivi karibuni. |
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha wanahabari wanawake nchini (TAMWA), Valerie Msoka alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu kuhusu harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia yaliyowashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ya kanda ya ziwa.
Msoka alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita waandishi wa habari walifanya kazi kubwa kwa jinsi walivyoandika habari na makala mbalimbali kupitia vyombo vyao wakielezea na kuielimisha jamii juu ya ubaya wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hali ambayo imechangia hivi sasa jamii kuwavichua watuhumiwa wa vitendo hivyo.
Alisema katika kipindi hicho TAMWA kwa upande wake ilijitahidi kuendesha mafunzo mbalimbali yaliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo waandishi waweze kuandika kwa ufasaha habari zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia sambamba na kuendesha tafiti nchi nzima ambako matukio ya ukatili huo yalibainika kuwepo.
“Binafsi nichukue fursa hii kuwapongeza waandishi wote ambao mmekuwa mkiandika habari na makala zinazoelezea matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na madhara yake, hali hivi sasa ni tofauti na huko nyuma, jamii imepata uelewa mpana na ndiyo maana imekuwa ikitoa taarifa kila pale vitendo hivyo vinapotokea,”
“Huko nyuma watu waliona aibu kutoa taarifa ya vitendo walivyokuwa wakitendewa, lakini kupitia kalamu zenu yapo mafanikio yameonekana, jamii imeanza kukemea vitendo hivi kwa mfano suala la ukeketaji dalili zinaonesha limepungua kiasi kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa na hata baadhi ya ngariba sasa wanajisalimisha,” alieleza Msoka.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alisisitiza suala la waandishi wa habari kujenga tabia ya kujiendeleza kwa kusoma badala ya kuridhika na elimu waliyonayo hivi sasa na kwamba mtu anayejiendeleza anakuwa na uwezo mkubwa wa kupanua kiwango chake cha uelewa ikilinganishwa na yule asiyetaka kujiendeleza.
“Ukisoma mtu unafungua akili na mawazo, unajiongezea hamu ya kufanya kazi lakini pia utaweza kujifunza kile ambayo ulikuwa hukijui katika kazi zako na hivyo kuweza kufanya kazi kwa ufanisi mzuri, TAMWA tunatoa mafunzo haya ili kila mwandishi awe na uelewa mpana katika kuandika habari za ukatili wa kijinsia,” alieleza Msoka.
Post a Comment