Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA), Valerie Msoka akizungumza na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga waliokuwa katika mafunzo ya jinsi ya kuandika habari zinazohusiana na matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
CHAMA cha Wanahabari wanawake nchini (TAMWA) kimependekeza katiba mpya ijayo iweke uwiano ulio sawa katika nafasi za ngazi za juu za uongozi wa serikali kwa lengo la kutekeleza mkataba wa Umoja wa Afrika (AU) unaotaka kuwepo kwa usawa kati ya wanaume na wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ya kanda ya ziwa jijini Mwanza, mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka alisema ni muhimu wajumbe wa bunge maalumu la katiba wahakikishe katiba mpya ijayo inatambua haki ya ushiriki wa wanawake katika uongozi wa nchi.

Msoka alisema wajumbe wa bunge la katiba wanapaswa kuelewa kuwa katiba ya nchi ni mali ya watanzania wote wanawake na wanaume, hivyo ni muhimu ikaweka msingi wa kumwezesha pia mwanamke kushiriki katika uongozi kwenye nyanja mbalimbali za kuteuliwa na kuchaguliwa.

“Sisi TAMWA na asasi nyingine za wanaharakati hapa nchini tunataka katiba mpya ijayo itambue haki ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na izuie kuhodhiwa kwa madaraka katika mihimili mikuu ya utawala na jinsi moja, tunataka ili kuweka usawa huo hivi sasa iwapo rais wa nchi atakuwa mwanaume, basi waziri mkuu awe mwanamke,”

“Iwapo utaratibu huu utazingatiwa ni wazi Tanzania tutakuwa tumetekeleza kwa vitendo mkataba wa Umoja wa Afrika (AU) ambao unataka nafasi za uongozi wa nchi iwe ni uwiano wa 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake, hii itafanya wanawake waweze pia kushiriki kwa uwiano ulio sawa katika mihimili mikuu ya kiutawala,” alieleza Msoka.

Msoka alisema ni vizuri pia  katiba mpya ijayo pawepo na kipengere kitakachovibana hata vyama vya siasa ili viweze kuweka ndani ya vyama vyao taratibu zitakazowawezesha wanawake kushiriki katika uongozi na kuwania nafasi za uwakilishi ndani vya vyama husika.

Katika hatua nyingine Msoka aliwaomba waandishi wa habari nchini kuendelea kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kalamu zao vinavyoendelea kutendeka katika maeneo mbalimbali na kwamba vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuielimisha jamii juu ya mambo mengi muhimu.

“Sisi TAMWA kama TAMWA hatuwezi kufanya kazi zetu peke yetu, ni lazima tushirikiane na wadau wengine wanaojishughulisha na masuala ya kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini, na wadau wetu muhimu ni waandishi wa habari, tunaamini kupitia kalamu zenu vitendo hivi vitapungua kama siyo kumalizika kabisa,” alisema
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top