Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akihutumia maelfu ya wakazi wa Mwanhuzi wilayani Meatu. |
Mbunge wa Kisesa akikabidhi pikipiki kwa mkuu wa sekondari ya Meatu Kapiga Shija baada ya kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kumaliza kidato cha sita. |
Onyo hilo limetolewa mjini Mwanhuzi na mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Juma Mwiburi maarufu kwa jina la mzee wa "jumla jumla" katika mkutano wa hadhara uliofanyika baada ya maandamano makubwa ya kumpokea mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) kwa ajili ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti wa moja ya kamati za kudumu za bunge.
Mwiburi alisema CCM wilayani Meatu imechoshwa na kitendo cha kushambuliwa kila wakati kwa matusi na mbunge huyo kila pale anapofanya mikutano yake ya hadhara jimboni ambapo badala ya kuwaeleza wananchi mambo gani ya maendeleo aliyowatekelezea hubaki akitoa matusi dhidi ya viongozi wa CCM, madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya.
Alisema iwapo mbunge huyo ataendelea na tabia hiyo viongozi wa CCM hawatosita kuomba ruhusa kutoka kwa viongozi wa ngazi ya juu ili na wao waanze kujibu mapigo na kwamba iwapo hali hiyo itatokea ni wazi mambo yatamwendea vibaya na atashindwa kumalizia vizuri kipindi chake kilichosalia.
“Kwa kweli viongozi na wanachama wa CCM sasa tumechoshwa na tabia ya mbunge huyu, maana kila anapofanya mikutano yake yeye agenda yake imebaki moja ni kutushambulia kwa matusi viongozi wa CCM, watendaji wa halmashauri yetu ya wilaya pamoja na madiwani, sasa tunamtumia ujumbe tunaomba aache mara moja,” alisema Mwiburi.
Naye mbunge Mpina ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge, Uchumi, viwanda na biashara alisema pamoja na jimbo la Meatu kuongozwa na mbunge kutoka chama cha upinzani, yeye binafsi atahakikisha anasimamia utekelezwaji wa miradi yote ya maendeleo iliyoahidiwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2010.
“Nawashukuru sana viongozi wa CCM walioandaa mkutano huu pamoja na madiwani tunaofanya nao kazi bega kwa bega kwa lengo la kuhakikisha maendeleo ya Meatu yanapatikana na mimi kama mbunge wenu nitahakikisha nalipigania jimbo la Meatu kwa nguvu zote ili kuona maendeleo yaliyoahidiwa yanapatikana,” alisema Mpina.
Alisema moja ya mambo aliyokwisha kufanyia kazi ni kuhakikisha serikali inakubali kutenga fedha katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoahidiwa kwa wilaya ya Meatu ikiwemo ile ya sekta ya kilimo, barabara, elimu na afya.
Mpina alisema kwa upande wa sekta ya kilimo amefuatilia suala la upatikanaji wa matrekta kupitia mpango wa kilimo kwanza na mpaka sasa trekta 20 zimeishasambazwa wilayani Meatu huku halmashauri kwa upande wake ikiwa tayari imedhamini trekta tatu kwa ajili ya vikundi vya kilimo.
“Pia nimemkumbusha Rais Jakaya Kikwete ahadi yake ya kutuwekea lami katika barabara za mji wa Mwanhuzi urefu wa kilometa tatu na kazi hiyo itaanza hivi karibuni, na lakini pia kazi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kolandoto, Meatu hadi mpakani mwa Arusha inatarajiwa kuanza kama CCM tulivyoahidi,” alisema Mpina.
Katika hatua nyingine Mpina alitoa zawadi ya pikipiki moja na shilingi milioni mbili kwa shule ya sekondari Meatu kutokana na kupata matokeo mazuri ya mitihani ya kumaliza kidato cha sita ikiwa ni mwaka wake wa kwanza tangu ilipoanza kutoa masomo ya kidato cha tano na sita.
"Ninawapongeza walimu wetu wa sekondari ya Meatu kwa kazi nzuri waliofanya, huu ndiyo mwaka wao wa kwanza tangu waanze masomo ya kidato cha tano na sita, lakini wanafunzi wamefaulu vizuri hakuna aliyefeli, hivyo nawazawadia pikipiki moja na shilingi milioni mbili ili zitengenezee vitanda vya hosteli, nasikia wanafunzi wameongezeka," alisema Mpina.
Post a Comment