Huu ndiyo mchuma waliokabidhiwa rasmi wachezaji wa timu ya Stand United Shinyanga baada ya kufanikiwa kupanda daraja na hivi sasa watacheza Ligi Kuu ya Vodacom. |
HATIMAYE mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini
(CCM) Steven Masele ametimiza rasmi ahadi yake ya kuipatia timu ya Stand United
basi dogo aina ya Coaster
litakalowasaidia kwa ajili ya usafiri wakati wakishiriki Ligi Kuu ya Vodacom.
Mbunge Masele aliwaahidi wachezaji wa timu hiyo
kwamba iwapo watafanikiwa kupanda daraja na kucheza ligi kuu ya Vodacom basi
mchango wake kwao itakuwa ni kuwapatia usafiri ili waweze kushiriki vyema
katika kinyang’anyiro hicho.
Basi hilo dogo lilikabidhiwa katika sherehe fupi za makabidhiano zilizofanyika katika viwanja vya kituo cha mabasi
yaendayo wilayani cha mjini humo ambapo mgeni rasmi alikuwa mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini, Kanali Maulid.
Akikabidhi rasmi basi hilo kwa viongozi wa timu
ya Stand United kwa niaba ya mbunge Masele ambaye hivi sasa yuko nje ya nchi
kikazi, Kanali Maulidi aliwapongeza wachezaji na viongozi wote wa timu hiyo kwa
jinsi walivyoweza kujituma na kufanikiwa kupanda daraja na hivyo mwaka huu
watacheza ligi kuu ya Vodacom.
“Nimekuja hapa kwa niaba ya mbunge wenu Steven
Masele, amenituma niwakabidhi msaada huu aliokuwa amewaahidi, leo hii ametimiza
ahadi yake, lakini name pia nitumie fursa hii kukupongezeni kwa juhudi zenu zilizowesha
mkafikia hatua hii, niwaombe msibweteke ili kuepuka kushuka daraja,”
“Sisi wakazi wa Shinyanga ahadi yetu ni kuendelea
kuwaunga mkono ili mshiriki vyema ligi hii ya Vodacom, CCM kwa upande wake tumewashauri
wenzetu wa manispaa waangalie jinsi gani watakusaidieni, maana sasa hii timu ipo
katika himaya yake, pale itakapokuwa ikicheza yapo mapato fulani yataingia
manispaa,” alieleza Kanali Maulid.
Awali viongozi wa timu hiyo, Amani Vincet
ambaye ni mwenyekiti na ofisa habari wa timu, Isaack Kisesa walimpongeza mbunge
Masele kwa kutimiza ahadi yake ambapo waliahidi kulitumia vizuri basi hilo
ambalo kwa kiasi kikubwa litawapunguzia tatizo la usafiri watakapokuwa
wakicheza michezo yao ya ligi ya Vodacom.
“Tuna kila sababu leo hii kumpongeza mbunge
wetu kwa kutimiza ahadi yake kwetu, lakini tuwaombe wadau wengine wa mchezo wa
mpira wa miguu hapa mkoani waendelea kujitokeza kutuchangia michango mbalimbali
ili tuweze kushiriki vizuri ligi hii, tuache kuweka siasa katika michezo, sisi
tunachoahidi ni kuhakikisha hatushuki daraja,” alieleza Vicent.
Mwisho.
Post a Comment