Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino katika moja ya mikutano ya chama hicho mjini Shinyanga.

KAULI iliyotolewa hivi karibuni na mbunge wa jimbo la Bumbuli na Naibu waziri wa Sayansi na Teknolojia nchini, January Makamba akidai Tanzania hivi sasa inahitaji Rais kijana imepokelewa kwa maoni tofauti na baadhi ya wanachama wa CCM mkoani Shinyanga.


Mmoja wa wanachama hao ambaye pia ni katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino alisema kauli ya Makamba aliyoitoa akiwa nchini Uingereza inaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM kwa vile inaonesha ubaguzi wa wazi kwa baadhi ya wanachama wake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga, Shigino alisema yeye binafsi anailaani kauli hiyo ambayo ameifafanisha na siasa za ubaguzi ndani ya chama na kwamba kutaka kulibagua kundi moja la wanachama walengwa wakiwa ni ni ubaguzi ambao haukubaliki.

Akifafanua katibu mwenezi huyo alisema, CCM daima imekuwa ikipinga suala la ubaguzi wa aina yoyote na kwamba kauli ya Makamba kutaka hivi sasa Rais ajaye mwaka 2015 atokane na vijana inaweza kusababisha mpasuko na mfarakano mkubwa ndani ya chama na pia inapingana na katiba ya CCM.

“Kwanza huyu bwana anapaswa aelewe kuwa ujana siyo kigezo cha sifa za mtu kugombea nafasi ya urais, nafasi hiyo ni nyeti ambayo mtu anayechaguliwa anapaswa awe ni mtu mwenye busara  na uwezo mkubwa wa kuongoza nchi bila kuyumba katika uongozi wake, wapo wazee wana uwezo mkubwa kuliko vijana,”

“Lakini pia kauli hiyo inapingana kabisa na katiba ya chama chetu, labda paitishwe mkutano mkuu tuweze kufanya mabadiliko ya katiba maana vinginevyo hoja ya ndugu yetu haitokuwa na mashiko iwapo wazee pia watajitokeza kutaka kuwania nafasi hiyo ya urais,"

"Katiba ya CCM Ibara ya 14 vifungu vidogo vya (1) hadi (3) vinafafanua wazi juu ya haki za mwanachama ikiwemo haki ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi, sasa hapa haijataja kwamba wenye haki hiyo ni vijana tu, inawezekana Makamba ametoa kauli hiyo kwa lengo la kutaka kuwatukana wazee kiungwana,” alieleza Shigino.

Alisema ni vizuri Makamba akakaa chini kwanza na kujifunza kutoka kwa wazee waasisi wa nchi hii ambao waliwahi kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa badala ya kutoa kauli ambazo zinaashiria mianya ya ubaguzi ndani ya chama na hivyo kuhatarisha mstakabali wa chama katika chaguzi zijazo.

“CCM ni chama kikongwe nchini ndani yake kuna akina mama, wazee na vijana wote hawa wana haki sawa kwa mujibu wa katiba yetu, mimi sioni tatizo la mgombea urais kwa tiketi ya CCM iwe atatokana na vijana au wazee, wote ni sawa mradi wawe na sifa na vigezo vinavyohitajika,” alisema.

Katibu mwenezi huyo ameviomba vikao mbalimbali vya uteuzi ndani ya CCM kupuuza kauli ya naibu waziri huyo na kwamba daima wajumbe wake watahadhari kuongozwa na matakwa ya watu bali wazingatie katiba na kanuni za chama katika uteuzi wao na muhimu kuangalia ni mtu gani mwenye uwezo wa kuivusha CCM bila kujali ni mzee au kijana.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top