![]() |
Majeruhi wa ajali wakipatiwa huduma ya kwanza katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga. |
WATU watatu wamekufa na wengine 45 wamejeruhiwa vibaya kufuatia ajali ya gari aina ya lori lililokuwa likisafirisha wafanyabiashara waliokuwa wakielekea mnadani Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuacha njia na kupinduka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema ajali hiyo imetokea huko katika barabara ya Shinyanga kuelekea Mhunze ikihusisha gari lenye namba za usajili T. 680 ARL aina ya Fuso lori lililokuwa na wafanyabiashara waliokuwa wakienda mnadani.
Kamanda Kamugisha aliwataja marehemu waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Charles Makengwa (30) mkazi wa kijiji cha Kiloleli, Difa Shimo (28) mkazi wa kijiji cha Bulimba wilayani Kishapu na mmoja ambaye mpaka jana mchana alikuwa hajatambuliwa jina wala makazi yake.
Akifafanua Kamanda Kamugisha alisema kati ya majeruhi waliojeruhiwa katika ajali hiyo 35 wamelazwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga na wengine 11 wapo katika hospitali ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga wakipatiwa matibabu.
Alisema mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa ambapo hata hivyo inahisiwa ni mwendo kasi na gari hilo ambalo linadaiwa lilikuwa limepakia abiria wengi na mizigo kupita kiasi.
“Inahisiwa chanzo cha ajali hii ni mwendo kasi, hivi sasa tunamtafuta dereva wa gari hilo aliyetajwa kwa jina la Ngassa Seni mkazi wa Kiloleli wilayani Kishapu ambaye alitoroka baada ya kusababisha ajali hiyo, tunaomba wananchi watusaidie kutoa taarifa popote watakapomuona ili aweze kukamatwa,”
“Jeshi la polisi tunatoa wito kwa wafanyabiashara kuacha tabia ya kupanda magari ya mizigo, na wamiliki wa magari hayo waache kupakia abiria, tumekuwa tukiwashauri mara zote magari ya mizigo yabebe mizigo na wafanyabiashara wapande magari ya abiria, waache ubahiri, wamiliki wa malori na wafanyabiashara wote watii sheria bila shuruti,” alisema Kamugisha.
Kwa upande wake Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa, Dkt. Daniel Magwija alikiri kupokea maiti tatu na majeruhi 35 ambapo sita kati yao wamelazimika kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Dkt. Magwija aliwataja majeruhiwa waliopelekwa Bugando kuwa ni pamoja na Caphrine Charles (24), Ndila Shigela (41), na Masanja Kishiwa (42) wote wakazi wa kijiji cha Mwajiginya wilayani Kishapu, Mayala Lugomela (31) na Michael Bundala wakazi wa Jijongo na Malando Mashamindi (20) mkazi wa Nhobola.
Post a Comment