Moja ya miradi inayodaiwa kutokamilika kikamilifu kutokana na kauli za wanasiasa kukataza wananchi kuchangia miradi hiyo - Pichani mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi (aliyejishika shavu) na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini Kanali Maulidi (mwenye shati la kitenge) wakisikiliza maelezo juu ya mradi wa maji katika vijiji vya Seseko na Mwamalili.
BAADHI ya viongozi wa kisiasa wametajwa kuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kutokana na kuwazuia wananchi kuchangia shughuli za maendeleo na kudai utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni jukumu la serikali.

Hali hiyo imebainishwa wiki iliyopita na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya manispaa walipokuwa wakitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika manispaa hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Shinyanga mjini waliokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.



Ilielezwa kuwa miradi mingi ya maendeleo imeshindwa kukamilika kwa wakati wake kutokana na wananchi kukataa kuchangia miradi hiyo huku wakidai serikali ndiyo yenye wajibu wa kuwaletea maendeleo wananchi wake na siyo kutafuta michango kutoka kwao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji katika vijiji vya Mwamalili na Seseko, Mhandisi wa maji manispaa ya Shinyanga, Nkinda Senni alisema mradi huo umeshindwa kukamilika kwa asilimia 100 kama ilivyokusudiwa kutokana na wananchi kusuasua katika ulipaji wa asilimia wanayopaswa kulipia kisheria.

“Huu mradi umepangwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 500, jamii kwa upande wao wanatakiwa kuchangia asilimia 2.5 ya gharama zote, lakini jambo la kusikitisha sehemu kubwa wameshindwa kutoa michango yao ambapo mpaka sasa kijiji cha Seseko kimechangia shilingi 650,000 na Mwamalili shilingi 500,000,”

“Kwa kawaida katika mradi huu jamii ilitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 19,985,265, lakini lengo limeshindwa kufikiwa kutokana na kauli za wanasiasa wanazozitoa majukwaani kudai serikali ndiyo yenye jukumu la kutekeleza miradi yote ya maendeleo, kuna hatari ya mradi huu kukwama iwapo fedha hazitapatikana,” alieleza Senni.

Hali hiyo ilijitokeza pia katika zahanati ya Kambarage ambako wajumbe hao wa CCM walielezwa kuwa pamoja na serikali kutoa wito wa wananchi kujiunga na Mfuko wa afya ya Jamii (CHF) lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa kikwazo kiasi cha wananchi kugoma kujiunga na mfuko huo.

“Mfuko wa afya ya jamii unakabiliwa na vikwazo vingi, mbali ya wananchi kuwa wagumu kujiunga na mfuko huu lakini pia wanasiasa wanachangia hali hii, mfano mzuri ni hapa kwetu tulipanga wajiunge kwa kulipia shilingi 10,000 kwa mwaka lakini wanasiasa walipinga na kutaka walipe shilingi 5,000, ni tatizo,” alieleza Dkt. Costantine Hubi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top