Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga akimpongeza mmoja wa askari polisi katika kituo cha Polisi cha Didia wilaya ya Shinyanga vijijini muda mfupi baada ya kukabidhi msaada wa mifuko 100 ya saruji iliyotolewa na mmoja wa wana CCM nchini kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi kata ya Didia

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amekanusha uvumi unaodai anakusudia kugombea ubunge katika Jimbo la Solwa na kuwataka wana CCM kutokuwa na hofu naye anapotembelea jimbo hilo.

Mgeja alibainisha hali hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali na wanachama wa CCM, wajumbe wa serikali za vijiji na kamati za maendeleo (WDC) katika kata ya Didia wilayani Shinyanga wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.


Alisema wapo baadhi ya watu wanaosambaza maneno yasiyo na ukweli kwamba yeye (Mgeja) amepanga kugombea ubunge katika jimbo la Solwa na kwamba kwenda kwake katika jimbo hilo ni sehemu ya maandalizi yake ya kutaka kugombea ubunge.

“Ndugu zangu nitumie fursa hii pia kuwaeleza ukweli kutoka ndani ya sahani ya moyo wangu kwamba mimi sina mpango wa kugombea ubunge katika jimbo hili la Solwa na sina mgombea ninayemuandaa, nilipogombea nafasi hii ya uenyekiti wa CCM mkoa nilitangaza wazi dhamira yangu ya kutaka kukijenga chama changu,”

“Nilieleza wazi kuwa kazi iliyo mbele yangu kwa sasa ni kukipingania na kukijenga chama changu na si vinginevyo, sasa haya maneno kwamba nina lengo la kugombea ubunge hapa yanatokea wapi? wapo watu hapa kila ninapokuja Didia wanafuatilia nyendo zangu kusikia eti nitazungumza kitu gani,”

“Wengine wanadai nataka kugombea ubunge kwa vile unalipa, siyo kweli maana hata bila ya ubunge mtu unaweza kufanya kazi zako na kujipatia kipato kuzidi cha mbunge, sasa ondoeni wasiwasi, tunapokuja huku lengo letu ni kusikiliza matatizo mliyonayo ili nasi tuwaelekeze watendaji wetu ndani ya serikali waweze kuyapatia utatuzi,” alisema Mgeja.

Mgeja alisema ni vizuri wana CCM wakawa makini nyakati za vipindi vya uchaguzi kutokana na watu wengi kutumia vipindi hivyo kuwachafua wenzao kwa kuwazuzishia mambo ambayo hayana ukweli wowote na badala yake wajikite katika kukiimarisha chama chao ili kiendelee kutawala.

“Wakati tukielekea katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ni muhimu wana CCM tukadumisha suala la umoja, mshikamano na upendo miongoni mwetu kwa maslahi na ushindi wa chama chetu, vipindi vya uchaguzi ni hatari sana, watu hupigana fitina mbalimbali kwa lengo la kuchafuana tu, tuwe makini,” alieleza Mgeja
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top