MUUNDO wa Serikali mbili unaopendekezwa na kundi la wengi ndani ya bunge maalumu la katiba umetajwa kuwa siyo utatuzi wa kero za muungano zilizopo hivi sasa nchini na kwa iwapo utapitishwa kuna uwezekano mkubwa wa muungano uliopo hivi sasa kuvunjika.

Hali hiyo imeelezwa wiki iliyopita na Naibu katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama huru vya wafanyakazi nchini (TUCTA), Hezron Kaaya alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi mkoani Shinyanga iliyoandaliwa na Mamlaka ya usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini (SSRA).

Kaaya alisema msimamo wa TUCTA ni kuwepo kwa muundo wa serikali moja ambao ndiyo utakuwa ufumbuzi wa matatizo na kero zote zilizomo ndani ya muungano na ni njia pekee ya kudumisha muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar zilizoungana mwaka 1964.

“Msimamo wetu TUCTA ni serikali moja, siyo mbili wala tatu, kwani pamoja na wale wanaopendekeza muundo wa serikali mbili zilizoboreshwa, wanapaswa waelewe kuwa bado tutaendelea na matatizo yetu tuliyonayo hivi sasa, siyo kweli serikali mbili zitakuwa mwisho wa kero za muungano, hili tunalipinga, suluhisho ni serikali moja,”

“Madai kwamba serikali mbili zilizoboreshwa ndiyo suluhisho la matatizo ya muungano siyo kweli kabisa, sanasana zitaongeza matatizo na ipo hatari ya kusababisha muungano wetu kuvunjika, ni vizuri wajumbe wa bunge la katiba wakawa makini katika kujadili suala hili bungeni, suluhisho ni kuwa na serikali moja wala siyo tatu,” alisema Kaaya.

Katika hatua nyingine naibu katibu mkuu huyo amewataka wafanyakazi nchini kuacha kutumika vibaya katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi mbalimbali ikiwemo wabunge na rais wa nchi ambapo alisema kitendo hicho kimechangia kupata viongozi wabaya wasiojali maslahi ya wananchi.

“Ndugu zangu wafanyakazi leo nataka niwaeleze kitu muhimu sana, hasa jamaa zangu walimu, kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kimewadia, sasa sisi wafanyakazi ni lazima tuwe makini sana, tutahadhari kutumika vibaya na wasaka nafasi za uongozi, tuhakikishe tunachagua viongozi imara na wachapa kazi wanaojali maslahi ya watu,”

“Mara nyingi tumekuwa tukitumika vibaya bila sisi wenyewe kujielewa, sasa katika chaguzi hizi zijazo tuwe makini tuhakikishe viongozi wote wababaishaji wasio na uwezo wa kuwatumikia watanzania bali kujali zaidi maslahi yao binafsi, hawa nasema hawatufai na hawastahili kuchaguliwa, tuwakatae wote wanaotaka kututumia kwa maslahi yao,” alieleza Kaaya.

Akizungumzia umuhimu wa wafanyakazi kujiunga na mifuko ya hifadhi alisema ni muhimu kwa vile ndiyo mkombozi mkubwa kwa wafanyakazi pale wanapostaafu na kuanza maisha ya uzee hali ambayo huwa na matatizo makubwa iwapo hawatakuwa na mafao yatakayowasaidia kumudu maisha ya kustaafu.

“Mimi niwaase wenzetu wanaobeza mifuko hii ya hifadhi ya jamii, maana kuna wanaotegemea kujipatia kipato kutokana na fedha za wizi au zile wanazopokea rushwa na hivyo kudai hawana haja ya kujiunga na mifuko ya hifadhi, lakini niwaeleze kuwa matumaini yao hayo ni bure, maana fedha yoyote inayopatikana kwa njia haramu, haina baraka,” alisema Kaaya.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top