SHINYANGA.
SAKATA la ongezeko la gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga limechukua sura mpya baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo kumtaka mkuu wa mkoa huo, Ally Rufunga atoe maelezo ya kilichosababisha kupanda kwa gharama hizo.
Hatua ya wajumbe hao wa CCM kutaka kupata maelezo kutoka kwa mkuu wa mkoa inatokana na malalamiko ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga kupinga viwango hivyo vipya vilivyoanza kutumika tangu Aprili mosi mwaka huu wakidai ni vikubwa na wapindashaji hawakuzingatia uwezo wa kipato cha wakazi wa mkoa huo.
Hali hiyo ilijitokeza juzi katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM mkoani humo baada ya kusomwa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM iliyoelezea hatua ya kupandishwa kwa gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa ikidaiwa ni agizo la serikali kwa lengo la kuifanya kuwa ya rufaa.
Wakichangia hoja katika kikao hicho baadhi ya wajumbe walidai huenda waliopanga ongezeko la viwango hivyo hawakitakii mema Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwamba gharama zilizoongezwa ni kubwa ikilinganishwa na hali halisi ya kipato cha wakazi wa mkoa wa Shinyanga kwa hivi sasa.
Mmoja wa wajumbe hao, Azza Hilal ambaye pia ni mbunge wa viti maalum, alisema kuna umuhimu wa viwango hivyo kupitiwa upya vinginevyo ipo hatari ya wananchi wengi kukosa imani na chama kinachoongoza serikali hali itakayosababisha wagombea wake katika uchaguzi mkuu ujao kuwa na wakati mgumu wakati wa kuomba kura kwa wananchi.
“Mheshimiwa mwenyekiti binafsi nimeshitushwa sana na taarifa ya ongezeko la gharama za matibabu katika hospitali yetu, leo mama mjamzito anatakiwa kulipa shilingi 70,000, hivi kwa mwanamke wa mkoa huu atazimudu vipi? Hapana lazima viwango hivi vipitiwe upya, tutawaumiza wananchi wetu,” alieleza Azza.
Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga alikiri kupokea malalamiko mengi ya wananchi wakipinga viwango hivyo huku wengi wao wakihoji iweje mkoa uwe na hospitali ya rufaa wakati wilaya zake karibu zote hazina hata hospitali za wilaya huku akidai wakati viwango hivyo vikitangazwa yeye alikuwa safarini.
Kutokana na hali hiyo mkuu huyo alitangaza kusitishwa mara moja kwa gharama hizo kuanzia jana baada ya kubainika kuwa viwango hivyo vilitangazwa bila kufuata utaratibu ambapo ilitakiwa mapendekezo yake yajadiliwa na vikao vya kamati za ushauri za wilaya (DCC) na baadaye yapate baraka za kikao cha Kamati ya ushauri ya mkoa (RCC).
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja aliwashukuru wajumbe kwa kuwa wazi na kulijadili suala la ongezeko la gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa bila woga na kwamba moja ya ahadi za CCM kwa wananchi wake ni pamoja na kuhakikisha inaboresha huduma za afya.
Aprili mosi mwaka huu, uongozi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga ulitangaza ongezeko la huduma za matibabu ambapo gharama za cheti zilipanda kutoka shilingi 1,000 hadi 5,000, gharama za kulazwa shilingi 5,000 kwa wiki moja badala ya shilingi 1,000.
Viwango vingine vilivyopandishwa ni ada ya vipimo vidogo vya damu (B/S) shilingi 2,000 kutoka shilingi 300, upasuaji mdogo shilingi 40,000 na mkubwa shilingi 80,000, kufanya tohara shilingi 40,000, ushonaji majeraha machache shilingi 20,000, kupasua jipu shilingi 40,000 na michubuko shilingi 10,000.
Post a Comment