Kahama
VIJANA nchini na watanzania wengine
wameshauriwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili waweze kujipatia ajira
halali badala ya kukimbilia kufanya shughuli ambazo mara nyingi huwangiza wengi
wao matatani ikiwemo uuzaji wa madawa ya kulevya.
Ushauri huo umetolewa juzi na mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi (CCM), Khamis Mgeja alipokuwa akikabidhi msaada wa TV yenye
thamani ya shilingi 260,000 kwa kijiwe cha uuzaji wa kahawa maarufu kwa jina la
BBC katika mji mdogo wa Isaka wilayani Kahama.
Mgeja alisema baadhi ya vijana wamekuwa
wakishawishika kupata utajiri wa haraka haraka na hivyo kujiingiza katika
shughuli zisizo halali ikiwemo uuzaji wa madawa ya kulevya tatizo ambalo
linaelekea kuwa sugu katika nchi hii na kuchafua sifa iliyokuwa nayo miaka ya
nyuma.
Alisema iwapo vijana katika nchi hii
watazitumia vizuri fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini wanaweza kujipatia
ajira zitakazowaingizia kipato kikubwa badala ya kufanya shughuli ambazo mara
nyingi husababisha waishie kufungwa gerezani.
Akifafanua alisema Tanzania ni moja ya nchi
duniani iliyobarikiwa kuwa na fursa kupitia sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi,
ujasiriamali mdogo na uanzishaji wa viwanda vidogo ambazo watanzania wanaweza
kuzitumia na kujipatia ajira bila ya kutegemea kuajiriwa ofisini na kujikwamua
kiuchumi badala ya kufanya kazi haramu.
“Ndugu zangu hasa ninyi vijana Tanzania tuna fursa nyingi iwapo zitatumika vizuri
mnaweza kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa ofisini, msiwe na tamaa ya
kupata utajiri wa haraka haraka bila ya kufanya kazi halali na badala yake
kukimbilia kazi haramu kama vile uuzaji wa madawa ya kulevya,”
“Maisha bora yaliyoahidiwa na serikali ya CCM
siyo kwamba yatadondoka kutoka mbinguni, hapana, bali ni kwa kufanya kazi,
tumieni fursa zilizopo, na sasa hivi mkoa wetu tuna viwanda vingi vipya vimejengwa
ni fursa pia ya kujipatia ajira, kazi ya serikali ni kuibua fursa, ninyi
mnazitumia,” alieleza Mgeja.
Awali akipokea msaada huo wa TV mwenyekiti wa
kikundi cha wajasiliamali hao wauza kahawa, Ali Msangi alimshukuru mwenyekiti
huyo wa CCM mkoani Shinyanga ambapo alisema msaada huo umefika wakati muafaka
kwa vile wataweza kufuatilia kwa kina mjadala wa rasimu ya pili ya katiba
unaoendelea hivi sasa bungeni.
Mwishoni mwa mwaka uliopita wajasiriamali hao
walimuomba mwenyekiti wa CCM mkoani humo aliyekuwa katika ziara ya kukagua
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 awasaidie kupata TV moja
itakayowasaidia kupata habari mbalimbali za dunia nyakati za asubuhi na jioni
ili waweze kuelewa yanayojiri ndani na nje ya nchi.
Post a Comment