Shinyanga
CHAMA Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA)
wilayani Shinyanga kimewashukia na kuwakemea viongozi wa CCM wakiongozwa
na mwenyekiti wao Taifa, Rais Jakaya Kikwete na kuwataka waache
kuwatisha wananchi juu ya muundo wa serikali katika katiba mpya
inayotarajiwa kupatikana nchini.
Chama hicho kimedai kuwa vitisho na kampeni za
waziwazi zinazoendelea kufanywa na wafuasi wa CCM hapa nchini vinaweza
kuchangia kwa kiasi kikubwa kutopatikana kwa katiba mpya inayotarajiwa na
watanzania wengi wanaopenda mabadiliko ambapo kimetahadharisha zoezi hilo lisiingize
nchi katika machafuko.
Hali hiyo imebainishwa juzi na viongozi wa
CHADEMA katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Ngokolo
mitumbani manispaa ya Shinyanga ambapo walisema kitendo cha Rais Kikwete
kupigia debe muundo wa serikali mbili kinapingana na sheria kwa vile tayari
kazi ya kujadili rasimu ya pili ya katiba imeanza kufanyika.
Mwenyekiti wa BAVICHA wilayani Shinyanga,
Hassan Barudi alisema Rais Kikwete hakupaswa kudharau na kuyaponda maoni ya
wananchi yaliyokusanywa na Tume Jaji Joseph Warioba kwa vile tume hiyo iliundwa
na yeye mwenyewe na maoni yaliyokusanywa ni ya watanzania wenyewe na siyo ya
Jaji Warioba kama inavyopotoshwa.
“Tunamshangaa sana Rais Kikwete kudai kuwa
serikali tatu haziwezekani, hii ni hofu isiyo na msingi kabisa, wenye nchi
ambao ndiyo waliomuweka madarakani wanadai muundo huo ndiyo bora, vipi kundi moja lipingane
na mawazo hayo, ni vizuri CCM wakaelewa kwamba wao hawana hatimiliki ya nchi
hii, hivyo wasiuteke mchakato wa katiba,”
“Mapendekezo ya muundo wa serikali ndiyo uamuzi
wa wengi, pia watanzania wanataka katiba mpya ijayo iweze kuruhusu Rais
atakayefanya vibaya katika utawala wake aburuzwe mahakamani badala ya kuendelea
kulipwa mafao yanayotokana na kodi za watanzania, tunaomba CCM wasituvuruge, katiba
mpya ni muhimu kwa mstakabali wa nchi yetu,” alieleza Baruti.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA wilayani
Shinyanga, Sili Yasini aliwaomba wakazi wa Shinyanga na watanzania kwa ujumla
kuwa makini wakati wa kipindi hiki cha mjadala wa rasimu ya katiba mpya
ukiendelea bungeni ili kuepuka nchi kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sili alisema wapo baadhi ya watu wanachukulia
suala la mabadiliko ya katiba kama jambo dogo na la kawaida ambapo busara
na hekima zisipotumika watanzania wanaweza kujikuta wakiingia katika vita vya
wenyewe kwa wenyewe kwa maslahi ya watu wachache wasiotaka kuachia madaraka
waliyonayo hivi sasa.
Alisema daima viongozi wa CHADEMA wataendelea
kupigania haki na maslahi ya watanzania bila kujali vitisho wanavyovipata kutoka
kwa viongozi wa CCM na kwamba hata kama viongozi wote ndani ya CHADEMA watauawa
lakini chama hicho kitaendelea kudumu wakati wote.
“Tuwaombe wajumbe wa bunge maalumu la katiba
watumie busara zao, wasiongozwe na maoni yanayotolewa na viongozi wa CCM hivi
sasa kudai maoni ya muundo wa serikali tatu ni ya Jaji Warioba, kama alivyosema
Kikwete mwenyewe, akili ya kuambiwa!!! Changanya na za kwako, wazingatie hilo,”
“Ni muhimu wakaongozwa na busara na hekima
zaidi kwa kuzingatia maoni ya watanzania, wakumbuke wamo ndani ya bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo halina itikadi yoyote ya chama cha siasa na siyo ndani
ya ukumbi wa CCM Chimwaga, vinginevyo wakivurunda na kuacha maoni ya watanzania ni wazi hawatawaelewa,” alieleza Sili.
Mwisho.
Post a Comment