Mauaji ya wanawake vikongwe na yale ya watu kujichukulia sheria mkononi yanaelekea kupamba moto mkoani Shinyanga baada ya watu wawili wengine kuuawa mmoja akituhumiwa kwa wizi wa kuku na mwingine kutokana na imani za kishirikina.
Mauaji hayo yametokea ikiwa ni wiki moja baada ya kutokea mauaji mengine kama hayo huko wilayani Kahama ambako wanakijiji wenye hasira walimshambulia kwa kipigo hadi kufa mkazi mmoja wa kijiji hicho Juma Masasila wakimtuhumu kutaka kumkata mapanga mkazi wa kijiji hicho.
Pia huko katika kijiji Mahengano wilayani Shinyanga kundi la watu wasiojulikana saa saba usiku wiki iliyopita walimvamia mkazi wa kijiji hicho aliyetajwa kwa jina la Misoji Kasubi (50) alipokuwa akienda kujisaidia na kumshambulia kwa kumkatakata mapanga hadi kufa.
Katika matukio mapya Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla amemtaja mtu wa kwanza aliyekufa kuwa ni Lucia Masunga (61) mkazi wa kijiji cha Nhelagani manispaa ya Shinyanga aliyeuwa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana.
Kamanda Mangalla alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 usiku wakati mwanamke huyo akiwa nje ya nyumba yake akiandaa chakula cha usiku ambapo alivamiwa na mtu wa watu wasiojulikana waliomshambulia kwa kumkata kata mapanga hadi kufa na kisha walitoweka bila ya kuiba kitu chochote.
Hata hivyo alisema mpaka hivi sasa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika japokuwa inahisiwa huenda yanahusiana na imani za kishirikina au ugomvi wa kuwania mali na hakuna mtu aliyekamatwa. Polisi inaendelea na uchunguzi.
Tukio la pili lilitokea huko katika kijiji cha Mawemilu kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga ambako kijana mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja mwenye umri kati ya miaka 25 na 35 aliuawa kikatili baada ya kushambuliwa hadi kufa na wanakijiji wenye hasira wakimtuhumu kuiba kuku wanne na kisha mwili wake waliuchoma moto.
Kamanda Mangalla alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11.45 jioni katika kijiji hicho baada ya wanakijiji kupiga yowe wakimtuhumu kijana huyo kuiba kuku hao wanne ambavyo hata hivyo mmiliki wake hajafahamika mpaka hivi sasa.
Hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo japokuwa kamanda huyo wa polisi amerudia kutoa wito anaoutoa mara kwa mara wa kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wanapowakamata watuhumiwa wawakabidhi mikononi mwa vyombo vya dola.
Post a Comment