Mbali ya kushamiri kwa mianya ya rushwa wakati Sumaye akiwa waziri mkuu, taasisi hiyo imedai kipindi chake ndipo Tanzania ilipofunga mikataba mingi mibovu iliyosababishwa na uwepo wa mianya ya rushwa mikataba ambayo mpaka sasa inapigiwa kelele na watanzania wengi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kijijini kwake Nyanhembe kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Mgeja alielezea kushangazwa kwake na kauli hiyo na kueleza siyo kweli Sumaye anaichukia rushwa kama alivyodai na kwamba anachokifanya kina lengo la kutaka kuwadanganya watanzania.
Alisema katika kipindi chake, Tanzania ndipo ilipofunga mikataba mingi mibovu katika sekta ya madini, viwanda, mashamba na ranchi za taifa ikiwemo uuzwaji wa benki ya umma (NBC) iliyouzwa kwa bei ya kutupa huku mwenyewe akijitwalia eneo kubwa la ardhi kule Kibaigwa mkoani Dodoma.
“Binafsi napingana na Sumaye katika hili, siyo kweli anachukizwa na tatizo la rushwa hapa nchini kama kweli angekuwa na sifa hiyo basi wakati wa kipindi cha uongozi wake asingeruhusu nchi yetu kufunga mikataba mibovu, leo hii watanzania wanalia kwa mikataba mibovu iliyofungwa wakati wake,”
“Katika kipindi chake rushwa ilikuwa kubwa sana, hata rushwa ya ngono ilishamiri wakati huo baadhi ya watendaji ndani ya serikali waligoma kutoa ajira mpaka mtu atoe rushwa ya ngono, kama anabisha mimi nitamtajia watu waliopewa ajira baada ya kutoa rushwa ya ngono, leo hii usafi anaodai anao uko wapi?” alihoji Mgeja.
Mgeja alisema ni vizuri badala ya kuhangaika Sumaye angekaa chini na kutulia badala ya kuwakumbusha watanzania machungu aliyowasababishia wakati akiwa kiongozi mkuu wa shughuli za serikali nchini ikiwemo pia ubinafsishaji wa mgodi wa Kiwira na uuzaji wa shamba la miti la Mgololo.
Alisema badala ya kulalamika angesaidiana na serikali juu ya mbinu gani zitumike katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili watanzania ili waweze kupata maisha bora wanayoyatarajia kinyume cha kudai anaichukia rushwa wakati aliiendekeza alipokuwa madarakani.
“Kwa kweli Sumaye hawezi kujigamba kwamba anachukia rushwa, kama kweli ana sifa hiyo, basi katika kipindi chake asingeruhusu mikataba mibovu ikiwemo ile ya Songas, IPTL, Meremeta, Mwananchi na wizi wa fedha za EPA, yote haya angezuia, aache kuwadanyanga watanzania,” alisema Mgeja.
Alimuomba aache kuwanyooshea vidole wenzake, na kuhoji nguvu hiyo anaipata wapi au ana lengo la kufunika madhambi yake aliyoyafanya wakati akiwa waziri mkuu, na kwa suala la rushwa hakuna mtanzania anayeliunga mkono maana wote wanakerwa na vitendo hivyo.
Pia Mgeja alitoa mfano wa maamuzi mabovu yaliyofanyika kipindi cha uongozi wa Sumaye kwa kuamua kuuza nyumba za umma zilizojengwa kwa nguvu ya watanzania wote wakiwemo wafugaji, wavuvi na wakulima ambao hawakushirikishwa katika kufikia maamuzi ya kuuzwa kwake na badala yake waliokumbuka ni wafanyakazi peke yao.
Alisema uingiaji wa mikataba mibovu inayoiumiza nchi hivi sasa ni rushwa kubwa kushinda rushwa ndogondogo anazozipigia kelele Sumaye zinazojitokeza mara nyingi nyakati za uchaguzi na kwamba huenda bado ana machungu ya kushindwa katika uchaguzi wa ujumbe wa NEC wilayani kwake ambako Mary Nagu alishinda.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari iwapo hivi sasa yupo katika harakati za kumfanyia kampeni mmoja wa watu wanaotaka kuwania urais nchini, Mgeja alisema yeye binafsi haamini kama ni wakati muafaka wa watanzania kuanza kulumbana juu ya mtu gani awe Rais mwaka 2015.
“Mimi nafikiri suala nani awe rais mwaka 2015 siyo wakati wakati hivi sasa, na halipaswi kupewa nafasi ya kusababisha watanzania tugawanyike, tujengeane uhasama, chuki na fitina na kusababisha kupoteza umoja na mshikamano wetu tulionao, maana urais unapangwa na mungu mwenyewe yeye ndiye anayemjua rais ajaye atakuwa nani,” alisema Mgeja.
Alisema suala la rais ajaye tayari limo ndani ya mioyo ya watanzania, ndiyo wanaojua ni nani atakuwa rais wao baada ya Rais Kikwete, hakuna sababu ya kulumbana na kwamba iwapo kelele za Sumaye ni juu ya kutaka kuwania urais mwaka 2015, ni vizuri akawaachia wananchi wenyewe ndiyo wataamua wakati utakapofika.
“Kama kelele hizi za mwenzetu ni urais wa mwaka 2015, tunamshauri aache kupapalika, akae chini atulie, na asiwasonte vidole vibaya wenzake, hakuna mtantania mwenye hatimiliki ya urais hapa nchini, wote wana haki sawa, ni juu ya watanzania wenyewe kuamua rais wao awe nani,” alisema Mgeja.
Post a Comment