mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Sylivestar Kasulumbai
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeiomba serikali ichukue hatua za makusudi za kuwasaidia wafugaji wa jamii ya kisukuma kwa kuwapatia maeneo ya ardhi yatakayowawezesha kuendesha shughuli zao za ufugaji bila ya kubughudhiwa. Ombi hilo limetolewa juzi na mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Sylivestar Kasulumbai alipokuwa akiwahutubia wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini humo. Kasulumbayi alisema hali ya wafugaji wenye asili ya kisukuma hapa nchini hivi sasa ni mbaya kutokana na mateso wanayoyapata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa serikali ambapo wamekuwa wakitimuliwa kila sehemu wanayokwenda ikidaiwa ng’ombe wao wanasababisha uharibifu wa mazingira na wengi wao wamejikuta wakikamatwa na kuwekwa ndani. Alisema kitendo cha kukamatwa na kunyang’anywa mifugo yao ni sawasawa na kuwalazimisha watu wa jamii ya wasukuma waendelee kuwa masikini kwa lazima watake wasitake na kwamba anachokizungumza siyo uchochezi kama ambavyo serikali ya CCM ilivyozoea kueleza kila pale watu wanaposema ukweli. Akifafanua mbunge huyo alisema hivi sasa kuna ng’ombe zaidi ya 12,000 huko katika wilaya ya Kaliua Tabora wanaoshikiliwa na maofisa wanyamapori ikidaiwa walikamatwa ndani ya eneo la hifadhi ambalo haliruhusiwi kuendeshea shughuli zozote za ufugaji kitu ambacho alikipinga kwa kudai ni cha ubaguzi. “Kwa kweli serikali ya CCM hivi sasa inataka kuwagawa watanzania na kama siyo kuwagawa basi inaendesha utawala wake kwa ubaguzi mkubwa, leo hii ng’ombe wa msukuma ni marufuku kuingia ndani ya eneo la hifadhi, lakini ng’ombe wa jamii ya kimasai kule Ngorongoro na Seregenti wao ruhusa kuchungiwa ndani ya hifadhi,” “Ni ajabu kuona ng’ombe wa wamasai wao hawaharibu mazingira, lakini wa wasukuma ndiyo waharibifu wa mazingira, nimepata taarifa hapa kuwa tayari kuna zaidi ya ndama 40 kati ya waliokamatwa wameisha kufa, hapana huu ni uonevu wa hali ya juu na ubaguzi wa aina yake, tunaomba serikali iliangalie tatizo hili,” alisema Kasulumbayi. Alisema kitendo cha serikali kuendelea kuwasumbua wafugaji hao wa kisukuma kinaweza kusababisha kutokea kwa vurugu kubwa hapa nchini pale wafugaji hao watakapochoka kuonewa, na kwamba serikali iache kutawala kiubauguzi, ielewe kuwa ng’ombe kwa jamii ya wasukuma ni M-Pesa na siyo chanzo cha uharibifu wa mazingira. Katika hatua nyingine wakazi wa jimbo la Shinyanga wametakiwa kukaa chini na kutafakari iwapo mbunge wao Stephen Masele (CCM) anatakeleza ahadi zake alizowaahidi baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri wa wizara ya nishati na madini nchini na kwamba kama ameshindwa kuzitekeleza ni vizuri wakaanza mikakati ya kumuondoa. “Wakazi wa Shinyanga mna kila sababu ya kuacha woga, hojini ahadi mlizoahidiwa na mbunge wenu wa CCM, inaonesha wazi ameshindwa kuzitekeleza na badala yake amediriki kuanza kuwatukana vijana ambao miongoni mwao ndiyo waliompigia kura, kataeni kudanganywa, fanyeni maamuzi sasa,” alieleza Juma Protas, mwenyekiti CHADEMA wilayani Kahama.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top