Shinyanga MWENYEKITI wa Serikali ya kijiji cha Songambele kata ya Salawe wilayani Shinyanga, Sekeyi Makonga juzi alijikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa kwa kipigo na ofisa wa serikali akiwa mbele ya ofisi za mkuu wa wilaya ya Shinyanga Hali hiyo iliyowashangaza watu waliokuwa katika eneo hilo ilitokea juzi saa 5.20 asubuhi baada ya ofisa huyo aliyetajwa kwa jina la James Kasigala ambaye ni ofisa ujenzi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kumkuta mwenyekiti huyo akiwa nje ya ofisi hizo za mkuu wa wilaya. Kitendo hicho kilisababisha ofisa huyo apelekwe mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya iliyokuwa ikiendelea na kikao chake ofisini kwa mkuu wa wilaya ambapo aliongozana na mwenyekiti aliyepigwa na baada ya maelezo ya pande zote mbili, mkuu wa wilaya aliagiza awekwe chini ya ulinzi na papo hapo alipelekwa mahabusu. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mwenyekiti huyo muda mfupi baada ya kushushiwa kipigo hicho ofisa huyo chanzo chake ni ofisa huyo kuchukizwa na kitendo cha kushitakiwa kwa mkuu wa wilaya kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji ikiwa ni kazi aliyokuwa ameahidi kuitekeleza. Akifafanua Makonda alisema ofisa huyo alikuwa amepewa kazi ya kusimamia ujenzi wa zahanati iliyokuwa ikijengwa katika kijiji chao cha Songambele lakini hata hivyo hakuwa makini katika usimamizi wake hali iliyosababisha kazi ifanyike chini ya kiwango na hivyo wanakijiji kulalamika. Kutokana na malalamiko hayo, kamati ya ujenzi inayoundwa na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga iliunda tume kufuatilia malalamiko ya wanakijiji hao ambapo ilibainika kuwa kutokana na usimamizi mbovu zahanati hiyo haikujengwa katika kiwango kinachohitajika na kiasi cha shilingi milioni 4.3 hazikutumika. Alisema baada ya kubainika hali hiyo, uongozi wa halmashauri ya wilaya ulimpa adhabu ofisa huyo ya kurekebisha kwa gharama zake mwenyewe mapungufu yote yaliyokuwa yamebainika katika ujenzi wa zahanati hiyo yaliyosababishwa na kushindwa kwake kusimamia kikamilifu ujenzi huo. Ilielezwa kuwa ofisi huyo alikubaliana na adhabu hiyo na alikwenda katika kijiji hicho kuanza kufanya marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza lakini hata hivyo alifanya kazi hiyo kwa muda mfupi na kisha aliondoka kijijini na uongozi wa kijiji ulipofuatilia aliwaomba wamvumilie kwa muda ili kwanza asafirishe wanae waliokuwa wakienda shule. Taarifa hiyo haikukubaliwa na wanakijiji ambapo walimtuma mwenyekiti wao aonane na mkuu wa wilaya ili amweleze hali halisi ya ofisa huyo kushindwa kumaliza kazi aliyokubali kuifanya ambapo mkuu wa wilaya baada ya kupata taarifa hiyo ndipo alipompigia simu na kumtaka afike ofisini kwake akiwa akiongozana na mkurugenzi mtendaji wake. “Sasa siku hiyo aliponikuta pale kwa mkuu wa wilaya ndipo alianza kunirushia maneno makali akidai nimekuwa nikimfuata fuata sana, ghafla alinirushia ngumi kama tatu hivi, nilijaribu kujitetea, tuliamriwa na baadae tuliitwa ofisini kwa mkuu, baada ya maelezo ya kutoa maelezo yetu iliagizwa akamatwe na awekwe ndani,” alieleza Makonga. Jeshi la polisi la polisi lilithibitisha kuwekwa mahabusu kwa ofisa huyo ambapo hata hivyo jioni mkuu wa wilaya aliagiza atolewa mahabusu ili kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za kazi zinavyoelekeza.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top