SERIKALI imeombwa kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kuwabaini baadhi ya wanunuzi wa madini ya dhahabu na almasi mkoani Shinyanga ambao wanajihusisha na utoaji wa taarifa za uongo kwa lengo la kukwepa kulipa kodi halali kutokana na madini wanayoyauza.
Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi kuwa baadhi ya wanunuzi wa madini hasa upande wa almasi wamekuwa wakifanya udanganyifu mkubwa na kukwepa kulipa kodi za serikali kila pale wanaponunua na kuuza almasi wanazozipata kutoka kwa wachimbaji wadogo katika machimbo ya Maganzo wilayani Kishapu na Mabuki mkoani Mwanza.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga waliozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni walisema kukosekana kwa usimamizi madhubuti kwa watu wanaonunua almasi kutoka kwa wachimbaji wadogo ni moja ya sababu inayochangia wanunuzi hao kukwepa kulipa kodi halali za serikali.
Wakazi hao walisema mara nyingi wanunuzi hao wamekuwa wakitoa taarifa za uongo juu ya mwenendo mzima wa biashara zao na serikali kujikuta ikipoteza mapato mengi kutoka katika sekta hiyo ya madini huku wanunuzi wenyewe wakipata faida kubwa.
Walisema pamoja na kuwepo kwa maofisa madini wenye jukumu la kuhakikisha wanunuzi hao wa madini wanafuata sheria za nchi, lakini bado baadhi yao pamoja na wale wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA) wamekuwa wakikubali kupokea taarifa hizo zisizo sahihi kwa maslahi yao binafsi.
“Baadhi ya wanunuzi wanaojihusisha na utoaji wa taarifa za uongo ili kukwepa kulipa kodi halisi ni raia kutoka nje ya nchi, hawana uchungu na nchi, sasa tabia hii inachangia kuhujumu uchumi wetu huku wao wakinufaika kutokana na pato wanalochuma hapa nchini,”
“Ni vizuri sasa serikali ikawamulika hawa watu, lakini pia ikawachunguza watumishi wake walioko katika idara ya madini iwapo kweli wanatimiza wajibu wao kikamilifu, maana bila hawa kuwa makini na wakweli, ni wazi serikali itaendelea kuondoka patupu kila siku,” anaeleza mmoja wa wachimbaji wadogo katika mji wa Maganzo Kishapu.
Kwa upande wake Bw. Ramadhani Hassan ambaye pia ni mkazi wa Maganzo wilayani Kishapu alisema moja ya mbinu inayotumiwa na wanunuzi wa madini ni kubadili mara kwa mara majina ya kampuni zao kwa lengo la kukwepa kodi za serikali.
Bw. Hassan alisema kwa kipindi kirefu ameshuhudia baadhi ya kampuni zinazomilikiwa na raia wa kigeni zilizopo mjini Shinyanga zimekuwa zikibadili majina ya kampuni pamoja na wakurugenzi wake kwa lengo tu la kukwepa kulipa kodi kutokana na mapato wanayopata kutoka katika madini ya almasi.
Alisema umefika wakati hivi sasa kwa serikali kutumia vyombo vyake vya kiusalama kuchunguza hali hiyo kwa pande zote mbili ikiwa ni kwa wanunuzi wenyewe na watumishi wa serikali waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kikamilifu.
Mwishoni mwa mwaka jana mmoja wa wanunuzi hao inadaiwa alinunua almasi ya karati 176 kutoka kwa wachimbaji wadogo huko katika machimbo ya almasi ya Mabuki wilayani Kwimba mkoani Mwanza na ikadaiwa kuwa hakuweza kulipa kodi halisi iliyotakiwa kutokana na thamani ya almasi hiyo kuwa kubwa.
Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dkt. Yohana Balele alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni alikiri kupatikana kwa almasi hiyo na kueleza kuwa taarifa zake zilifikishwa wizarani.
Dkt. Balele alisema baada ya kupatikana kwa taarifa za almasi hiyo muhusika alifuatiliwa ambapo aliipeleka wizarani na ikafanyiwa tathimini juu ya thamani yake halisi kwa lengo la kukokotoa kodi iliyopaswa kulipwa na mmiliki wake na kwamba kodi yote ililipwa.
Mbali ya hali hiyo, mkuu huyo aliahidi kufuatilia madai ya wananchi ya kuwepo kwa baadhi ya wanunuzi wanaokwepa kulipa kodi za serikali kutokana na madini wanayonunua kutoka kwa wachimbaji wadogo na kwamba watakaobainika atahakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha Dkt. Balele aliahidi kufanya uchunguzi kuhusiana na malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakidai kuwepo kwa kampuni moja inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika pori la hifadhi ya Taifa la Kigosi wilayani Bukombe mkoani Shinyanga ambapo kampuni hiyo imedaiwa kuacha kufanya kazi ya utafiti na badala yake kuchimba dhahabu.
Mwisho.
Post a Comment