Kishapu
WANANCHI wakazi wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga wameiomba serikali iwapelekee msaada wa haraka wa chakula ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili hivi sasa.

Ombi la wananchi hao linatokana na sehemu kubwa ya Jimbo la Kishapu kukabiliwa na ukame kutokana na kutokunyesha kwa mvua za kutosha katika msimu wa mwaka huu na kusababisha mazao mengi ya wakulima kukauka mashambani.

Wakizungumza katika mikutano tofauti ya hadhara iliyofanyika juzi katika vijiji vya Masanga, Kisesa na Kinampanda wilayani humo wananchi hao walimuomba mbunge wa jimbo hilo, Bw. Suleiman Nchambi awafikishie kilio chao serikalini ili waweze kusaidiwa chakula cha msaada.

Walisema kutokana na uhaba wa chakula unaowakabili hivi sasa, baadhi ya kaya zimekuwa zikishindia mlo mmoja kwa siku na wengine kulazimika kutumia uji pekee kutokana na kutokuwa na chakula na pia uhaba wa fedha za kuwawezesha kununulia chakula kutokana na kupanda bei.

“Mheshimiwa mbunge tunakushukuru kwa kutukumbuka kuja kutushukuru baada ya sisi kukupigia kura zetu na ukaweza kushinda, lakini tunachokuomba utusaidie tuweze kupata msaada wa chakula, hali ni mbaya, ukame uliojitokeza katika msimu wa mwaka huu umetuathiri na kusababisha mazao yetu kukauka mashambani,” alieleza Bi. Sofia Gamaya.

Akijibu ombi hilo, mbunge wa jimbo hilo, Bw. Nchambi aliwaagiza maofisa watendaji wote wa vijiji vilivyoathiriwa na ukame kufanya tathimini sahihi ili kuweza kubaini kiwango cha msaada wa chakula unaohitajika katika maeneo yao.

“Ni kweli jimbo letu maeneo mengi linakabiliwa na ukame wa kutisha, na mazao mengi yamekauka, lakini ili tuweze kupata msaada wa serikali ni muhimu sasa kwa watendaji wa vijiji wakashirikiana na wale wa kata kufanya tathimini haraka juu ya mahitaji halisi ya msaada unaohitajika kwa kubaini kaya zote zinazohitaji kupatiwa msaada ili tuweze kuwasilisha serikalini,” alieleza Bw. Nchambi.

Aidha kwa upande mwingine mbunge huyo aliwaagiza maofisa ugani wa kata kufanya tathimini na kumpelekea taarifa juu ya mbegu bora za mazao mbalimbali yanayostahimili ukame ikiwemo mtama ili aweze kutafuta mbegu hizo kwa ajili ya kuwapatia wakulima wa jimbo la Kishapu.

Bw. Nchambi alisema hali ya hewa katika maeneo mengi imebadilika katika siku za hivi karibuni na hivyo kuhitajika kufanyika kwa utafiti wa kutosha ili kuweza kubaini ni mbegu zipi zikipandwa zitaweza kuhimili hali ya ukame uliopo katika jimbo hilo.

Mbunge huyo yupo katika ziara ya kutembelea kata na vijiji mbalimbali kwa lengo la kusikiliza matatizo ya wananchi ili aweze kuyafanya kazi sambamba na kutoa shukrani zake kwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Kishapu.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top