Februari 04, 2011.
Shinyanga
WAKATI Shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) likiongeza makali ya mgao wa umeme kwa wateja walioko katika gridi ya Taifa, wateja wa mjini Shinyanga wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watumishi wa shirika hilo kugeuza suala la mgao kuwa mradi wa kujipatia fedha.

Hatua hiyo inatokana na shirika hilo kutokuzingatia ratiba ya mgao kama ambavyo ulivyotangazwa kupitia katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini baada ya kuelezwa kuwepo kwa matatizo katika mitambo ya kuzalisha umeme.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti jana mjini Shinyanga, wateja hao walidai pamoja na kuwepo kwa ratiba ya mgao wa umeme lakini watumishi wa TANESCO hawafuati ratiba hiyo kutokana na kuyapendelea baadhi ya maeneo ya watu wazito kifedha.

Wateja hao walisema utaratibu wa mgao unaonesha kuwa kila eneo litakuwa likizimiwa umeme kwa masaa 10 nyakati za mchana na masaa matano kwa usiku kwa kupishana siku, lakini utaratibu huo haufuatwi kutokana na baadhi ya maeneo wanakoishi wananchi wa kawaida kuzimiwa umeme kila siku nyakati za usiku.

Walisema kwa kawaida iwapo eneo moja linazimiwa umeme tangu saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni, siku inayofuata eneo hilo hilo hutakiwa kuzimiwa umeme kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 5.00 usiku.

“Sasa ajabu sisi watu wa maeneo ya viwandani kwa siku tatu mfululizo tumekuwa tukizimiwa umeme kuanzia saa 12.00 mpaka saa 5.00 usiku, lakini ajabu maeneo ya mjini kati na kwa watu wazito hawa kwa siku zote hizo wamekuwa wakipata umeme kutwa nzima bila ya kuzingatia ratiba ya mgao.

“Tumejaribu kuulizia tukaelezwa kuwa sisi kwa vile eneo letu lipo katika viwanda, eti wenye viwanda wameomba kuwa wanawashiwa umeme nyakati za mchana na uzimwe usiku, hili ni tatizo,”

“Vipi wathaminiwe wenye viwanda na wananchi wa kawaida tuwe gizani kila siku kwa sababu yao, ina maana waliopanga suala la mgao hawakufahamu kuwa kuna maeneo ya viwanda?” alihoji mmoja wa wateja waliolalamikia hali hiyo.

Aidha yapo madai kuwa baadhi ya mitaa ambayo hapo awali ilikuwa ikiingizwa katika mgao wa kawaida hivi sasa njia yao imebadilishwa na kuunganishwa katika njia ya hospitali na maeneo nyeti kama vile polisi na nyumba za ibada.

Maeneo hayo kwa kawaida hayapaswi kuwa na mgao kutokana na umuhimu wake na kuhitajika muda wote yawe na umeme, lakini kwa mswahili wa kawaida kuunganishwa katika njia hiyo ni wazi inaashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa.

Hata hivyo kaimu meneja wa TANESCO mkoani Shinyanga, Bw. Sanibella Mahenge alikanusha madai ya kuwepo kwa mianya ya rushwa katika suala la mgao wa umeme ambapo alisema kuongezeka kwa makali ya mgao huo kunatokana na matatizo yaliyopo katika mitambo inayosambaza umeme nchini.

“Si kweli kwamba kuna upendeleo katika ugawaji wa umeme, hapana, juzi kulitokea tatizo kule eneo la Ndembezi, ilibidi tuzime umeme ili kurekebisha hitilafu iliyojitokeza, lakini kwa mchana huo eneo hilo halikuwa katika ratiba ya kuzimiwa, hivyo tukaona tuwashe viwandani na usiku tuzime na tuweze kuwawashia wala wa eneo hilo la Ndembezi,”

“Bahati mbaya sana siku ya Alhamisi, Februari 3, 2011 tukapokea maelekezo mapya ya mgao wa kitaifa, ikabidi tupange ratiba mpya, lakini ratiba hiyo pia ikawa inaangukia watu wa viwandani wazimiwe umeme usiku,”

“Na hata leo (Ijumaa 4.02.2011) bado pia tutawazimia usiku wateja wetu wa eneo la viwandani, hii ni baada ya kuagizwa sasa mgao utakuwa ni wa kila siku badala ya ule wa kwanza, kwa wapo watakaokuwa wakizimiwa nyakati za asubuhi kwa masaa 10, na usiku masaa matano,” alieleza Bw. Mahenge.

Mwisho.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top