Shinyanga
BODI ya Maendeleo ya Waislamu mkoani Shinyanga imetoa tamko lake kwa niaba ya waislamu wengine kuhusiana na mjadala unaoendelea hivi sasa hapa nchini wa watanzania kuhitaji kuandikwa kwa katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Shinyanga mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Sheikh Mohammed Issa alisema wakati mchakato wa kuhitajia uwepo wa katiba mpya ni vizuri pakawepo na maandalizi ya kutosha yatakayotoa nafasi sawa kwa watanzania wote kuweza kutoa maoni yao bila ubaguzi.
Sheikh Mohammed alisema kufuatia mjadala wa katiba mpya ulioibuka kwa nguvu hapa nchini wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, watu mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya katiba.
Alisema waislamu kama kundi jamii la kidini kati ya makundi mawili makuu ya kidini hapa nchini ambayo ni waislamu na wakristo, wanayo haki ya kutoa maoni yao kama raia wa Tanzania kuhusu mjadala wa katiba unaoendelea hivi sasa.
“Maoni yetu kuhusu mjadala wa katiba mpya ni kwamba, mosi waislamu tunaunga mkono kwa dhati tamko la Rais Jakaya Kikwete kuhusu hitajio la katiba mpya ya nchi yetu, pili, tunaona mjadala wa katiba unachukua mwelekeo ambao si sahihi kwa uzoefu wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya katiba ya nchi yoyote duniani,”
“Mjadala wa katiba mpya unaelekea kutekwa au kuhodhiwa na watanzania wachache tu waishio mijini wakiwemo wanasiasa, wanataaluma na vikundi vya kijamii, sehemu kubwa ya watanzania waishio vijijini imeachwa nyuma,”
“Wananchi waishio vijijini na hata mijini hawajui kabisa katiba ya sasa na inaelekea kutokujua kwao kunachukuliwa kama sababu halali ya kutowahusisha katika mjadala huu unaoendelea hivi sasa,”
“Mtazamo huu si sahihi kwani vijijini kuna wasomi wengi tu kama vile walimu wa shule za msingi na sekondari zilizopo vijijini, wataalamu wa huduma mbalimbali kama vile ugani, afya, jamii na wengineo wengi,” alieleza Sheikh Mohammed.
Mwenyekiti huyo alisema upo umuhimu mkubwa kwa jamii inayoishi vijijini ikahusishwa kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusiana na katiba mpya inayotaka kuandikwa hivi sasa ikiwa ni pamoja na makundi yote ya kidini yaliyopo nchini.
“Sisi Bodi ya maendeleo ya waislamu Shinyanga, tunaitaka serikali kuuendea mchakato wa kuleta katiba mpya kwa umakini mkubwa, usawa na uadilifu ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na katiba itakayopatikana inakuwa kwa maslahi ya watanzania wote si chama au kikundi fulani cha watu,” alieleza.
Alifafanua kuwa mabadiliko ya katiba ndiyo njia bora kabisa ya waislamu hapa nchini kudai haki zao za msingi walizokuwa wakizilalamikia likiwemo suala la mahakama ya kadhi na kwamba mahakama hiyo lazima iwepo katika katiba itakayokuja vinginevyo waislamu hawataelewa kitu.
Sheikh Mohammed aliwataka wale wote watakaojadili katiba mpya wafanye hivyo bila dharau, ubaguzi wala chuki kwa watanzania wengine, kila kundi jamii liachwe lieleze lenyewe linataka katiba mpya iseme nini katika yale masuala yanayolihusu.
Pia makundi jamii mengine yaheshimu matakwa ya kundi jamii hilo ilimradi hayavunji haki za msingi za binadamu wengine au imani yao, na itakapotokezea kutofautiana, basi mazungumzo ya amani kati ya pande mbili zinazotofautiana iwe ndiyo suluhisho pekee la kuondoa utata huo.
“Kwa kuelewa umuhimu wa katiba katika maisha ya raia, tunawahimiza waislamu wote Tanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kudai katiba kama wadau muhimu katika mchakato huo na kamwe wasiwe wasindikizaji,” alieleza Sheikh Mohammed.
Post a Comment