CHAMA Cha walemavu wa ngozi albino (TAS) mkoani Shinyanga kimeiomba wizara ya afya nchini kuacha utaratibu wa kuwafanyia majaribio walemavu wa ngozi kwa vile majaribio hayo yanaweza kuwasababishia madhara makubwa.
Hatua ya chama hicho inafuatia kitendo cha wizara ya afya hivi karibuni kusambaza mafuta yanayotumika kwa ajili ya walemavu wa ngozi kujikinga na mionzi ya jua ili kuyafanyia majaribio kama yanafaa.
Mafuta hayo yanayodaiwa kusambazwa kwa vyama vya walemavu wa ngozi kote nchini ni aina ya ENAT Natural vitamin E Cream kutoka nchini Australia ambayo yameletwa hapa nchi ili kufanyiwa majaribio kuona kama yanafaa kuyatumia katika kujikinga na mionzo ya jua.
Wakizungumza na waandishi wa habari ofisini kwao jana viongozi wa TAS mkoani Shinyanga walisema baada ya kupokea mafuta hayo na kujaribu kuyatumia wamebaini yana madhara makubwa kwao na kwamba hayafai kutumia na albino hapa nchini.
“Kwa kweli haya mafuta hayafai, tumejaribu kuyatumia lakini wengi wetu yamewaletea matatizo makubwa, baada ya kuyapaka wanavimba mwili wote na kupasuka pasuka ngozi, sasa tumebaini kuwa hayatufai,”
“Jambo la kusikitisha ni kuona wizara ya afya imedai kuwa mafuta haya yameingizwa hapa nchini kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, sasa hii ni hatari, iweje viongozi wetu wakubali kuleta kitu kwa ajili ya kutufanyia majaribio sisi, tunaomba hii tabia ikome,” alieleza mwenyekiti wa TAS mkoa wa Shinyanga, Bi. Eunice Zablon.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji ya TAS mkoa wa Shinyanga, Bw. Elia Zablon alisema mafuta hayo waliyopewa kwa ajili ya kufanyia majaribio yamemsababishia madhara makubwa na hayafai kutumiwa na walemavu wa ngozi hapa nchini na kwamba ni bora waendelee kupata madhara ya mionzi ya jua kulikoni kutumia mafuta hayo.
“Haya mafuta hayafai kabisa, hawa watu wanataka kutumia ngozi zetu kwa ajili ya majaribio yao, hawafahamu kuwa wanaweza kusababisha vifo vyetu, ni bora tuendelee kupata mafuta ya ng’ombe kulikoni kutumia msaada huu wa bure ambao una madhara makubwa kwetu,” alieleza Bw.
Kwa upande wake katibu wa mkoa wa chama hicho Bw. Lazaro Anaely alisema chama chake kinatarajia kutoa elimu ya afya juu ya kujikinga na mionzi ya jua kwa albino wa wilaya ya Bukombe, Meatu, Kishapu na Manispaa ya Shinyanga.
Bw. Anaely alisema mradi huo umefadhiliwa na Shirika la misaada la The Foundation for Civil Society kwa kiasi cha shilingi milioni 44 mradi ambao utaendeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuwafikia walengwa 200 wakiwemo watumishi wa idara ya afya, polisi na waandishi wa habari mkoani Shinyanga.
Post a Comment