(Pichani Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dkt. Yohana Balele akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga).


Kishapu, Shinyanga.

MADIWANI katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wametakiwa kusimamia vyema mapato na matumizi ya fedha za wananchi katika Halmashauri hiyo na kuepusha vitendo vya wizi vilivyokuwa vimeshamiri katika Halmashauri hiyo.

Agizo hilo lilitolewa juzi na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dkt. Yohana Balele alipokuwa akizungumza na madiwani wapya wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu katika semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Kishapu.

Dkt. Balele alisema Halmashauri ya wilaya ya Kishapu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita iliongoza katika vitendo vya wizi wa fedha zilizokuwa zikikusanywa katika Halmashauri hiyo kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri.

Alisema wapo watendaji wasio waaminifu ndani ya Halmashauri hiyo ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya madiwani kuhujumu fedha za wananchi wa Kishapu ambapo katika kipindi hicho zaidi ya shilingi bilioni moja zilipotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Tafadhali sana ndugu madiwani hivi sasa mnaanza kazi mpya, hakikisheni mnasimamia vizuri fedha zinazokusanywa katika halmashauri yenu na zile za ruzuku zinazotolewa na serikali, wapo miongoni mwenu waliokuwa wakishirikiana na watendaji kuiba fedha za umma, nasema waache mara moja,” alieleza Dkt. Balele.

Dkt. Balele alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya Kishapu Bw. Theonas Nyamhanga kutoa taarifa kwa madiwani kila anapopokea fedha za ruzuku kutoka serikali kuu na kwamba madiwani watapaswa kufahamu kiasi halisi cha fedha kilichopokelewa na miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha hizo.

“Tangu sasa ni juu yako mkurugenzi kuwafahamisha madiwani juu ya fedha zote ulizopokea au kukusanya kutoka mapato ya ndani, na madiwani ni juu yenu kuhakikisha fedha hizo zinatekeleza miradi iliyopangwa na kwa kiwango kinacholingana na fedha hizo,”

“Halmashauri ya Kishapu ina rekodi mbaya ya upotevu wa fedha za umma, mwaka jana tumefanya ukaguzi wa ghafla katika miradi kadhaa tulikuta maajabu, kuna eneo ilielezwa katika taarifa mmechimba bwawa, lakini tulipokwenda hatukukuta bwawa, tafadhali jisahihisheni,” alieleza Dkt. Balele.

Kwa upande mwingine mkuu huyo mkoa amewataka madiwani kujiepusha na tabia ya kufanya biashara pamoja na Halmashauri, na kwamba vitendo hivyo vimekuwa vikichangia miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango kinachotakiwa, na hakuna hatua zinazochukuliwa kwa vile wahusika ni madiwani wenyewe.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top