Shinyanga
BAADHI ya wakazi wa mji wa Shinyanga wamemshauri Rais Jakaya Kikwete kutoa tamko rasmi kwa kumtaja mmiliki wa kampuni ya Dowans Holdings ili watanzania waweze kumfahamu kabla ya kuanza kutekeleza hukumu ya kuilipa kampuni hiyo kiasi cha shilingi 185 bilioni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Majira juzi mjini Shinyanga wakazi hao walisema pamoja na kwamba Mahakama ya kimataifa ya kusuluhisha migogoro ya kibiashara (ICC) kuipa ushindi kampuni hiyo na kuitaka TANESCO kulipa kiasi hicho cha fedha lakini mpaka hivi leo watanzania hawamfahamu mmiliki wa Dowans.

Walisema ni jambo la ajabu na la kushangaza kuona shirika la serikali ambayo ni halali linapelekwa mahakamani na mtu ambaye hajulikani na serikali inakubali haraka haraka kutaka kulipa adhabu iliyotolewa na mahakama hiyo ya usuluhishi ambapo haifahamiki ni mtu yupi atakayelipwa fedha hiyo.

“Kwa kweli umefika wakati kwa Rais Kikwete sasa abebe jukumu la kuwafahamisha rasmi watanzania mmiliki halisi wa Dowans, itakuwa ni miujiza na aibu kwake kulipa fedha hizo kwa mtu asiyejulikana, watanzania hatujawa wajinga kiasi hicho, kila mara serikali imekuwa ikieleza wazi kutomfahamu mmiliki wa Dowans,”

“Sasa kama mmiliki huyo hafahamiki fedha ambayo waziri mkuu hivi karibuni amenukuliwa na vyombo vya habari akikiri kuwa lazima serikali ilipe itazipeleka kwa mtu gani? Rais atueleze na amtaje huyo mtu, vinginevyo watanzania hatutokubali fedha hiyo ilipwe, na hata ikilipwa kwa nguvu waelewe iko siku tutaidai kwao,” alieleza Bw. Fredy Mmassy.

Bw. Mmassy alisema mbali ya Rais Kikwete kumtaja mmiliki wa kampuni hiyo pia awaeleze watanzania ni mwakilishi yupi wa serikali aliyeiwakilisha TANESCO katika mahakama hiyo ya usuluhishi (ICC).

Alisema pia serikali inapaswa sasa kuweka wazi mkataba uliofungwa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Richmond pamoja na ule wa Dowans ili kila kitu kiweze kufahamika na watanzania wajionee wenyewe ni wapi TANESCO inapotiwa hatiani.

Kwa upande wake mkazi wa kitongoji cha Ndembezi Bw. Masunga Jilaba alisema mbali ya Rais Kikwete kumtaja mmiliki wa kampuni ya Dowans lakini pia aingilie kati mara moja kuzuia ongezeko la bei ya umeme lililotangazwa kuanza rasmi mwezi ujao.

Bw. Jilaba alisema kitendo cha ongezeko la bei ya matumizi ya nishati ya umeme kwa asilimia 18.5 kinaonesha wazi jinsi gani wateja wa TANESCO ndiyo wanaopaswa kuilipa kampuni hiyo ya Dowans ambayo mtu hahitaji kuwa na elimu ya chuo kikuu kufahamu kuwa ni kampuni ya mfukoni.

“Tunaomba Rais Kikwete kama kweli anawathamini watanzania waliomchagua kwa moyo mmoja hivi karibuni basi azuie ongezeko la bei mpya za umeme hapa nchini, viongozi wetu waziri mkuu na hata waziri Ngeleja wameonesha wazi kutokuwa na huruma na watu wao, wanakubali kulipa shilingi bilioni 185 na kuongeza bei ya umeme,”

“Hawa wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu hawatoi hata chapa moja mifukoni mwao kwa ajili ya kulipia umeme, sasa uchungu wataupata wapi, ni watanzania masikini hawa wanaohangaikia hata mlo wao wa siku ndiyo watapaswa kulipa deni hilo la Dowans kupitia Ankara za kila mwezi za matumizi ya umeme,” alieleza Bw. Jilaba.

Wakati huo huo serikali imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kusitisha mikataba yote na makampuni ya uzalishaji umeme ikiwemo ile ya IPTL na Songa’s na fedha ambayo sasa inalipwa kila siku kwa makampuni hayo kama Capacity charge itumike kwa ajili ya kununulia mitambo itakayomilikiwa na serikali.

“Umefika wakati sasa wa serikali kukatisha mikataba mibovu inayowakamua watanzania katika suala zima la uzalishaji wa nishati ya umeme hata kama ni kulipa fidia basi fidia ilipwe ili fedha zinazolipwa kila siku kwa makampuni hayo ielekezwe katika kununua mitambo yetu sisi wenyewe,”

“Hii watanzania tutakuwa radhi hata kama nchi itaingia gizani kwa miezi miwili mfululizo ni bora iwe hivyo, na katika kipindi hicho umeme mchache unaozalishwa na TANESCO yenyewe uelekezwe katika maeneo nyeti tu ya uzalishaji, ili mradi tu baada ya muda mfupi tuwe na mitambo yetu wenyewe,” alieleza Bw. Juma Shukuru.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top