Shinyanga
KAULI ya mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema kuhusiana na suala la malipo ya shilingi bilioni 185 kwa kampuni ya Dowans na madai ya kuandikwa upya kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokelewa kwa maoni tofauti na wakazi wa Shinyanga.
Wakati baadhi ya wakazi wa mji wa Shinyanga wakimtaka mwanasheria mkuu kujiuzulu wadhifa wake, wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa huenda anatumika vibaya pasipo yeye mwenyewe kujielewa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Majira mjini hapa jana wakazi hao walisema kitendo cha Jaji Werema kufunga mjadala wa malipo ya Dowans ni sawa na kutumia ‘udikiteta’ katika jambo ambalo wananchi walipaswa kufahamishwa undani wake kwa kina kabla ya malipo.
Walisema madai yaliyotolewa na Jaji Werema kwamba baada ya kuipitia na kuisoma hukumu iliyotolewa na Mahakama ya kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Biashara (ICC) amekubali kuwa hukumu hiyo iko sahihi ni sawa na kuwauza watanzania.
“Kwa kweli hapa mwanasheria wetu ameonesha wazi kuwa ameshindwa kutumia wadhifa wake katika kuitetea nchi, wapo watu wanafikishwa mahakamani kwa makosa halisi kabisa, lakini bado wanakana kutenda makosa hayo kwa nguvu zote, na wakati mwingine wanashinda kesi,”
“Leo mwanasheria wetu anakubali virahisi tu kwamba hukumu hiyo ni sahihi, tunauliza kwa misingi ipi, nani mmiliki wa Dowans basi kama Bw. Rostam Aziz aliyekuwa akitajwa tajwa kudaiwa kuwa yeye alipewa nguvu tu ya kisheria na siyo mmiliki wa Dowans, sasa tutajiwe ni nani mwenye hiyo Dowans, Werema (Jaji) si amtaje?” alihoji Bw. Khalid Kyaruzi.
Naye Bw. Shabani Ramadhani mkazi wa mjini Shinyanga alidai kuwa tamko la Jaji Werema limeonesha wazi jinsi gani asivyokwenda na mkuu wake wa kazi aliyemteua katika wadhifa huo na hana uchungu na nchi yake.
Bw. Ramadhani alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliyemteua Jaji Werema katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu nchini aliwaeleza watanzania kuwa serikali ya CCM ni serikali sikivu, hivyo aliwaomba waendelee kuipa ridhaa ya kuongoza nchi.
“Sasa huyu bwana hataki watanzania tuendelee kuhoji suala la Dowans, anasema mjadala umefungwa, huku ni kupingana na ‘boss’ wake, Rais Kikwete aliisha tueleze kuwa serikali yake ni serikali sikivu, inawajali na kuwasikiliza wananchi wake,”
“Kama ni sikivu mbona haisikilizi kilio hiki cha wananchi cha kugoma kulipwa kwa malipo hewa kwa kampuni ambayo serikali yenyewe imeshindwa kumuweka wazi hadharani mmiliki wake, lakini ajabu pia huyu bwana hataki hata katiba yetu iandikwe upya ili iweze kuendana na wakati, sasa serikali hii kweli ni sikivu?” alihoji Bw. Ramadhani.
Kwa upande mwingine mmoja wa watumishi wa serikali mkoani Shinyanga ambaye hakupenda kutajwa jina alidai kuwa kitendo cha Jaji Werema kukataa kuwepo kwa katiba mpya hapa nchini kinaonesha jinsi gani mwanasheria huyo asivyoweza kwenda na wakati.
“Watanzania wote pamoja na baadhi ya viongozi wastaafu na walioko madarakani wanakubali kuwa suala la katiba mpya linazungumzika, lakini mwanasheria wetu anakurupuka na kudai kuwa hakuna haja hivi sasa ya nchi kuandika katiba mpya, nafikiri huyu bwana anatumika vibaya,” alieleza mtumishi huyo wa umma.
Mtumishi huyo alishangazwa na kauli ya Jaji Werema kwamba katiba iliyopo inastahili kuendelea kuwepo na kwamba kama suala la masahihisho ni bora kufanyike marekebisho katika baadhi ya vipengere badala ya kuandikwa mpya ambapo alitoa mfano wa katiba ya nchi ya India ambayo amedai imefanyiwa marekebisho zaidi ya mara 50.
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa Baraza la wa wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Shinyanga ambaye hakupenda pia kutajwa gazetini amemuomba Rais Kikwete akubali kulizungumzia suala la malipo ya shilingi bilioni 185 kwa kampuni ya Dowans kwa kumtaja mmiliki wake.
Mzee huyo alisema kama kweli Rais Kikwete anawajali watanzania waliomchagua hivi karibuni basi ajitokeze hadharani na kutoa tamko na kwamba moja ya madai ya Spika mstaafu Bw. Samwel Sitta ni kwamba Dowans haikustahili kulipwa malipo hayo kwa vile ilidandia mkataba kutoka kwa kampuni iliyoshindwa kutekeleza mkataba wake kisheria.
Post a Comment