Shinyanga

WAKAZI wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake wamekumbwa na wasiwasi mkubwa kutokana na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Shinyanga mjini, Bw. Festo Kang’ombe kutoweka ofisini kwake katika mazingira ya kutatanisha.

Hatua ya kutoonekana ofisini kwa Bw. Kang’ombe kwa muda wa siku nne sasa kumetafsiriwa kuwa kutokana na kutangaza matokeo yenye utata ya wagombea ubunge katika jimbo la Shinyanga.

Mpaka jana mchana Bw. Kang’ombe alikuwa hajaonekana ofisini kwake na hata pale wasaidizi wake wa karibu walipohojiwa alipo walikuwa na majibu mafupi ya kusema, “…subirini, hayupo mbali atakuja sasa hivi.”

Inadaiwa kuwa baada ya msimamizi huyo kutangaza matokeo kwa kushinikizwa na viongozi wa CCM, aliamua kutoroka kwa kuruka senyenge zilizozungushwa katika ofisi yake ambapo usiku wa Novemba mosi mwaka huu inasemekana alilala wilayani Kahama kwa ajili ya kunusuru maisha yake.

Waandishi wa habari waliofika katika ofisi za Manispaa mjini hapa kufuatilia matokeo halisi ya uchaguzi katika jimbo hilo hawakuweza kufanikiwa kukutana na msimamizi huyo japo mtu aliyekuwa akikaimu baadhi ya shughuli za ofisi Bw. Boniphace Maheli alidai hakuwa mbali angefika ofisini wakati wowote.

“Ndugu zangu mimi ninasaidia shughuli ndogo ndogo za kiofisi lakini mambo yote yanayohusu masuala ya uchaguzi na matokeo ya uchaguzi huo msubirini mwenye ofisi, ndiye mwenye mamlaka ya kuyazungumzia kwa mujibu wa sheria, muda mfupi atakuja ofisini fanyeni subira,” alijibu Bw. Maheli majibu ambayo amekuwa akiyarejea kila mara alipoulizwa na waandishi wa habari.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri ya manispaa hiyo wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina yao walidai hivi sasa ofisi ya mkurugenzi huyo haieleweki kutokana na kitendo cha kukaimishana bila kufuata utaratibu.

Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mgombea ubunge katika jimbo la Shinyanga yaliyomtangaza mgombea wa CCM Bw. Steven Masele kuwa ndiye mshindi kwa kupata kura 18,570 dhidi ya kura 18,569 alizopata mpinzani wake kupitia chama cha CHADEMA, Bw. Philipo Shelembi ikiwa ni tofauti ya kura moja.

Hata hivyo matokeo yanayodaiwa pia kutolewa na msimamizi huyo wa uchaguzi yanaonesha kuwa Bw. Masele wa CCM alipata kura 18,750 na Bw. Shelembi wa CHADEMA alipata kura 18,507 ikiwa ni tofauti ya kura 243.

Hali hiyo ilisababisha wafuasi wa CHADEMA kuingia mitaani kupinga matokeo hayo ambapo katika vurumai zilizotokea baada ya matokeo kutangazwa zilisababisha kuchomwa moto kwa ofisi ya mkurugenzi wa manispaa iliyokuwa ikitumika kama ofisi yaTume ya uchaguzi.

Kuchomwa moto kwa ofisi hiyo kulisababisha kuteketea kwa masanduku yote ya kupigia kura ikiwemo kura za urais, ubunge, udiwani na kumbukumbu nyingine muhimu za uchaguzi huo.

Tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza adhima yake ya kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo wakidai kupokwa kura zao ambapo kinadai matokeo yaliyopatikana kutoka vituo vya kupigia kura yanaonesha Bw. Shelembi alipata kura 19,231 na Bw. Masele kura 19,010.

Mbali ya madai ya kupokwa kura zao pia wanalalamikia kukiukwa kwa taratibu kadhaa katika zoezi zima la uhesabuji wa kura kutoka vituoni na kwamba katika hali isiyokuwa ya kawaida, msimamizi wa uchaguzi hakuweza kutangaza kura za urais wala idadi ya watu waliopiga kura na kura zilizoharibika.

Mbali ya hali hiyo mpaka jana mchana hapakuwa na matokeo yoyote ya uchaguzi wa wabunge na yale ya urais yaliyobandikwa katika mbao za matangazo za Manispaa ili wananchi waweze kuyaona kama sheria za uchaguzi zinavyoelekeza.

Juhudi za kumpata msimamizi huyo wa uchaguzi zilishindikana pamoja na kupigiwa simu yake ya mkononi iliyokuwa muda wote ikiita bila kupokelewa.

Hata hivyo katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga, Bi. Mwamvua Jilumbi alikanusha uvumi wa kutoroka kwa Bw. Kang’ombe na kwamba bado yupo kazini na hajajiuzulu kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

“Huyu bwana yupo kazini, mimi mwenyewe nimezungumza naye jana (juzi) kwa simu, lakini leo hii ameondoka mjini hapa kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake, hajajiuzulu yuko kazini kama kawaida,” alieleza Bi. Jilumbi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top