Shinyanga

HALI ya utulivu katika manispaa ya Shinyanga kwa siku tatu mfululizo mara baada mara ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mbunge imeendelea kuwa tete kutokana na wananchi kupinga matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini yaliyomtangaza mgombea wa CCM, Bw. Steven Masele kuwa ni mshindi huku masanduku yote ya kura yakiteketea kwa moto.

Kutokana na hali hiyo juzi jioni mara baada ya matokeo hayo kutangazwa watu wasiojulikana waliamua kuichoma moto ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa iliyokuwa ikitumika kwa kazi ya kujumlishia matokeo ya kura za urais, ubunge na madiwani.

Moto huo uliteketeza masanduku yote ya kura za urais, ubunge na madiwani zilizokuwa zimepigwa katika Jimbo la Shinyanga mjini pamoja na kumbukumbu zote muhimu ikiwemo kompyuta iliyotumika kuingizia matokeo katika mtandao wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Bw. Selemani Nyakipande alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mpaka jana mchana hapakuwa na mtu ye yote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo .

Hata hivyo jana mnamo saa sita mchana baadhi ya shughuli za kibiashara katika mitaa ya soko kuu mjini Shinyanga zililazimika kufungwa kufuatia jeshi la polisi kuendelea kufyatua mabomu ya machozi ovyo katika maeneo mbalimbali ambapo walikuta pakiwepo mkusanyiko wa makundi ya watu.

Hali hiyo ilisababisha malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi ambao walidai Jeshi la polisi lilikuwa likitumika vibaya kutaka kuwashinikiza wananchi wakubali matokeo ambayo si halali na kwa mtu ambaye hawakumchagua

Akizungumzia hali hiyo ya ufyatuaji ovyo wa mabomu Bw. Nyakipande alisema ilisababishwa na baadhi ya vijana kuwarushia mawe baadhi ya polisi waliokuwa wakilinda hali ya usalama mitaani na kuashiria kufanya vurugu mitaani wakipinga matokeo hayo ya uchaguzi, japo alisema mpaka kufikia saa saba mchana alikuwa ameagiza kusitishwa kwa zoezi la ulipuaji wa mabomu.

Wananchi hao walishauri serikali iangalie uwezekano wa kubadili utaratibu wa kuwapata wabunge katika nchi hii kwa kuweka utaratibu mpya wa kuwateua kama inavyofanya kwa wakuu wa mikoa na wilaya badala ya kupoteza bure fedha za walipa kodi wa Tanzania kwa ajili ya uchaguzi ambao matokeo yake yanachakachuliwa.

“Hakuna haja ya kuwa na uchaguzi katika nchi hii kama hali ndiyo hii, maamuzi ya wananchi yanaonekana wazi hayathaminiwi, iweje chombo cha dola kishinikize kukubaliwa kwa matokeo, wakati wapiga kura wameona wazi kumefanyika hujuma,”

“Hapa demokrasia haipo, ni bora wabunge nao wateuliwe kama wakuu wa mikoa na wilaya, upigaji mabomu ovyo mitaani ni kupoteza hela za umma bure mbali ya kuwasababishia matatizo wazee, wagonjwa na watoto,” alieleza Bw. Nyamongo mkazi wa manispaa ya Shinyanga.

Pamoja na polisi hiyo jana mchana kuendelea kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kutawanya makundi ya wananchi katika maeneo mbalimbali mjini hapa, hali hiyo haikusaidia kitu kutokana na wananchi kuonesha wazi kuyazoea mabomu hayo ambapo kila yalipopigwa wananchi walitawanyika kwa muda na baadae kurejea.

Hata hivyo baadhi ya wananchi walionesha wasiwasi wao kutokana na uchomwaji moto wa ofisi za mkurugenzi wa manispaa kutokana kuhisi huenda ikawa ni hujuma iliyofanyika makusudi baada ya kubaini kura zilizohesabiwa hazikuwa halali na hivyo wahusika kuamua kuzichoma moto ili kupoteza ushahidi.

“Kwa kweli hii ni hujuma ya wazi, jana (juzi) baada ya matokeo kutangazwa na wananchi kuonesha kutoyakubali polisi walifyatua mabomu na wakaondoka kabisa katika eneo hili, lakini ajabu wakati polisi wakiwa wameimarisha ulinzi kuzunguka majengo yote ndipo tukio la moto lilipotokea, ni wazi si wananchi waliouwasha moto huo,” alieleza mwananchi mmoja

Juhudi za kumpata mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga kuzungumzia tukio hilo zilishindikana baada ya kuelezwa kuwa alikuwa safarini wilayani Kahama, na hata pale simu yake ya kiganjani ilipopigwa ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.

Waandishi wa habari walishuhudia watumishi wa manispaa hiyo jana wakishindwa kufanya kazi yoyote ile kutokana na kuungua kwa moja ya majengo ya ofisi zao ambapo hata mkurugenzi mwenyewe wa Manispaa Bw. Festo Kang’ombe ilielezwa kuwa alilazimika kwenda kulala wilayani Kahama kwa ajili ya usalama wake.

Wananchi hao juzi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais, ubunge na madiwani huku yakiwa yamecheleweshwa walipinga matokeo hayo na kudai kuwa msimamizi wa uchaguzi alishinikizwa kumtangaza mgombea wa CCM, Bw. Steven Masele aliyedaiwa kupata kura 18,750 ambapo yule wa CHADEMA, Bw. Philipo Shelembi alipata kura 18,507.

Hata hivyo tayari viongozi wa CHADEMA wameyakataa matokeo hayo na wanakusudia kukata rufaa kuyapinga ambapo mbali ya kiti cha ubunge pia wamepinga matokeo ya kiti cha udiwani katika kata mpya ya Lubaga.

Katibu wa CHADEMA mkoani Shinyanga Bw. Nyangaki Shilungushela alisema mbali ya kupinga matokea ya ubunge pia watapinga matokeo ya udiwani katika kata ya Lubaga ambako mgombea wa CHADEMA awali alitangazwa kuwa mshindi lakini baadae alienguliwa na kutangazwa mgombea wa CCM kuwa ndiye mshindi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top