Shinyanga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini kimekanusha uvumi wa mbunge aliyechaguliwa hivi karibuni katika Jimbo la Shinyanga mjini kwa tiketi ya CCM, Bw. Steven Masele kulikimbia jimbo lake.

Hatua hiyo inafuatia baadhi ya wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake kueneza uvumi wakidai Bw. Steven Masele ameamua kulikimbia jimbo lake muda mfupi mara baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kote Oktoba 31, mwaka huu.

Hata hivyo matokeo hayo katika jimbo la Shinyanga mjini yalikuwa na utata mkubwa baada ya mpinzani wa Bw. Masele aliyekuwa amegombea pia ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA Bw. Philipo Shelembi kuyapinga.

Utata huo wa matokeo ya kiti cha ubunge katika jimbo la Shinyanga mjini ulisababisha pia msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika jimbo hilo Bw. Festo Kang’ombe ambaye ni mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kutoweka kazini kwake katika mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu katibu wa CCM wa wilaya ya Shinyanga mjini, Bw. Saidi Bwanga alikanusha uvumi huo na kueleza kuwa wanaovumisha ni watu wasiomtakia kheri Bw. Masele pamoja na Chama chake cha Mapinduzi.

“Kwa kweli mbunge wetu hajakimbia jimbo, ni uvumi tu usiokuwa na maana yoyote, wengi wanaouvumisha wanatoka katika kambi ya upinzani, ni moja ya kujaribu kuzima aibu ya kushindwa kwao, wanadai mgombea wetu hakushinda, lakini sisi tunaamini alishinda,” alieleza Bw. Bwanga na kuongeza,

“Sasa wanataka kuipotosha jamii kwa kudai kuwa mbunge amekimbia jimbo, wapo wanaodai akitoka Dodoma anapitiliza Dar es Salaam, na wengine wanadai amehamishia familia yake mkoani Morogoro, madai haya si kweli, huyu bwana akitoka Dodoma atarejea Shinyanga, na pia atapita kila kata kuwashukuru wananchi,” alieleza.

Aidha Bw. Bwanga ambaye pia ni katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini amewaomba wanachama wa CCM na wapenzi wa Chama hicho kupuuza uvumi huo na kwamba wajiandae kumpokea mbunge wao pale atakapokuwa akirejea kutoka Dodoma .

Kwa zaidi ya wiki moja sasa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake kumezagaa uvumi unaodai kuwa Bw. Masele amehamisha familia yake kwa lengo la kulikimbia jimbo, na kwamba baada ya kuapishwa kuwa mbunge rasmi hivi sasa makazi yake yatakuwa jijini Dar es Salaam na kwamba hatua hiyo inatokana na ushindi usiokuwa wa uhakika.

Katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni mgombea wa CCM, Bw. Steven Masele alitangazwa kuwa mbunge katika Jimbo la Shinyanga mjini baada ya kupata kura 18,570 ambapo mpinzani wake Bw. Shelembi wa CHADEMA alipata kura 18,569.

Hata hivyo matokeo hayo bado yana utata mkubwa kutokana na kuwepo matokeo mengine yakidai Bw. Masele alishinda baada ya kupata kura 18,750 na Bw. Shelembi alipata kura 18,507 matokeo ambayo yalipingwa vikali na mgombea wa CHADEMA akidai mshindi katika uchaguzi huo alikuwa ni yeye.

Kwa upande wake mgombea wa CHADEMA Bw. Shelembi alidai yeye ndiye aliyepaswa kutangazwa mshindi baada ya kupata kura 19,231 ambapo Bw. Masele wa CCM alipata kura 19,010 matokeo ambayo yanadaiwa kupatikana kutoka katika vituo vya kupigia kura.

Wakazi wa jimbo hilo la Shinyanga mpaka hivi sasa wameshindwa kupata uhakika wa matokeo ya uchaguzi wa mbunge katika jimbo lao kutokana na msimamizi msaidizi katika jimbo hilo kushindwa kubandika matokeo rasmi katika mbao za matangazo kama sheria za uchaguzi zinavyoelekeza.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top