SOLWA SHINYANGA - KAMPENI ZA JAKAYA


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya kazi kubwa itakayofanywa na serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kumsaidia mkulima wa Tanzania aweze kulima kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono.

Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Lyabukande, jimbo la Solwa wilayani Shinyanga katika moja ya mikutano yake ya kampeni iliyofanyika jana.

“Katika miaka mitano ijayo iwapo mtatupa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, tumepanga kumsaidia mkulima ili aweze kuboresha kilimo chake kwa kumuwezesha kulima kwa trekta badala ya jembe la mkono alilolizoea enzi na enzi,” alieleza Rais Kikwete.

Alisema iwapo mkulima atasaidiwa katika kilimo chake, ataweza kujikomboa kutokana na umasikini na kumuwezesha kuwa na maisha bora kama ambavyo sera ya CCM inavyoelekeza.

Pia Rais Kikwete alisema katika kukabiliana na tatizo la maji linalowakabili wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga, tayari serikali imeagiza vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 15 kutoka linapopita bomba kuu la maji kutoka Ziwa Victoria vipatiwe maji.

Akiwahutubia wakazi wa mjini Shinyanga juzi jioni Rais Kikwete alisema serikali tayari imeanzisha mradi maalumu wa ujenzi wa nyumba za askari polisi na wale wa jeshi la wananchi (JWTZ) ili kupunguza tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi kwa askari hao.

Rais Kikwete alisema katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za makazi kwa polisi na askari wa jeshi la wananchi, serikali iliamua kuanzisha mradi huo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo kwa nchi nzima.

“Tumeanzisha ‘project’ maalumu kwa ajili ya askari wetu wa jeshi la wananchi na polisi, tayari mradi huu umeanza baada ya kukopa fedha kutoka kwa wahisani,”

“Hata hivyo hivi sasa tunaongea na wahisani hao kuona uwezekano wa kutupunguzia riba ya mkopo huo, tunataka tuombe zaidi ya mara tano ili tuweze kujenga nyumba nyingi za kutosha na kuzikarabati zilizopo ziwe na hadhi,” alieleza.

Kwa upande mwingine Rais Kikwete alisema baada ya kukamilisha mradi mkubwa wa kitaifa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Shinyanga na Kahama, hivi sasa serikali yake inafanya kila juhudi ili kuwezesha kufufuliwa kwa kiwanda cha nyama kilichopo nje kidogo ya mji wa Shinyanga.

Alisema pamoja na kwamba hivi sasa serikali haifanyi biashara lakini itasaidia kutafuta mwekezaji atakayeweza kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho cha nyama ili kiweze kufanya kazi ambapo pia kitachangia kutoa ajira kwa wakazi wa Shinyanga.

Aidha Rais Kikwete alisema iwapo wananchi watakubali kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, atahakikisha anaendeleza na kukamilisha miradi yote ya maendeleo iliyokwisha anzishwa na kuongeza mingine mipya kwa kadri ya hali itakavyokuwa.

“Nilikuja hapa mwaka 2005, mliniomba niwasaidie ukamilishaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, tayari umekamilika, palikuwa na kero ya madaraja ya Ndala na Mshikamano, kazi imekamilika, hospitali ya mkoa, ukarabati mkubwa umefanyika na kuwekwa vifaa vya kisasa,”

“Zaidi ya shilingi bilioni mbili zimetumika kwa ajili ya ukarabati huo, nab ado tunaendelea tunataka sasa iwe hospitali ya rufaa ya mkoa mtu akitoka hapa akimbizwe Bugando au Muhimbili,” alieleza Rais Kikwete.

Katika hatua nyingine wakazi wa mkoa wa Shinyanga wamempongeza na kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi alivyoweza kuwatekelezea sehemu kubwa ya ahadi alizoziahidi alipokuwa akipita kuwaomba kura mwaka 2005.

Shukrani hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) za kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho iliyofanyika katika miji ya Mwanhuzi, Lalago, Malampaka na Shinyanga mjini.

“Mheshimiwa Rais Kikwete watu wa mkoa wa Shinyanga wanakushuru sana kwa jinsi ambavyo umeweza kutekeleza ahadi zako ulizowaahidi mwaka 2005 ulipokuja katika mkoa wetu kuomba kura za urais,”

“Tayari hivi sasa kero ya maji imekwisha katika miji ya Shinyanga na Kahama baada ya kupata maji kutoka ziwa Victoria, na pia barabara yetu kuu imejengwa kwa kiwango cha lami na mambo mengi ya kimaendeleo yamefanyika. Kule Meatu pia walikuwa na tatizo la maji sasa hivi limekwisha, tunakushuru,”

“Tunakushukuru sana na tunakuombea mungu uzidi kutuongoza, na wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga wameahidi kukupa kura zao zote Oktoba 31, mwaka huu,” alieleza Bw. Hamisi Mgeja mwenyekiti wa CCM wa mkoa.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top